BUNGE LARIDHIA AZIMIO LA SADC



Watanzania wengi wataweza kufanya biashara na kuwekeza katika nchi za Kusini mwa Afrika kuanzia sasa.
Hatua hiyo inatokana na Bunge kuridhia juzi jioni Itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ya Fedha na Uwekezaji, yaani SADC Protocol on Finance and Investment.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyesoma Azimio la kuridhia Itifaki hiyo ya SADC juzi asubuhi. Alisoma Azimio hilo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya.
Nchemba alisema lengo la itifaki hiyo ni kuweka mazingira bora ya sera za fedha na uwekezaji kwa nchi wanachama ili yaendane na malengo makuu ya SADC, ikiwemo mzunguko huru wa mitaji, bidhaa, nguvukazi na huduma.
Akiwasilisha Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu Azimio hilo, Mjumbe wa Kamati hiyo, Said Mussa Zubeir  alisema suala la kuwa na sarafu moja ya SADC kwa wanachama ifikapo mwaka 2024, linapingana na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuwa na sarafu moja kwa nchi wanachama ifikapo mwaka 2018.
Akichangia, Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia alihoji ni kwa nini imechukua muda mrefu kuridhia Azimio hilo la kimataifa. Alisema kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuridhia itifaki hiyo ya kimataifa.
 “Tuache maneno kama Taifa, tuangalie cha kufanya. Tanzania ni nchi ya pili duniani baada ya Brazil kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo kuna haja ya kuangalia jinsi ya kuwekeza katika utalii,” alisema Mbatia ambaye ni Mbunge wa chama cha NCCR-Mageuzi.
Aidha, Mbatia aliiomba Serikali iwezeshe Watanzania wengi kuanzia sasa kuwekeza katika nchi hizo za SADC.
Mchangiaji mwingine, Dk Mary Nagu alisema kuridhiwa kwa itifaki hiyo ya SADC, kuna manufaa mengi, kama vile kuwawezesha Watanzania kuwekeza katika nchi yoyote mwanachama wa SADC. Pia, sasa Watanzania wataweza kufanya biashara katika mataifa hayo ya SADC.
Dk Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji, alisema SADC ina watu milioni 300 na eneo kubwa lenye vivutio vingi vya kiuchumi, hivyo kuna umuhimu kwa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.
Nchi za SADC ni pamoja na Malawi, Zambia, Swaziland, Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe, Tanzania, Lesotho, Mauritius na Madagascar.

No comments: