Wizara ya Afya Zanzibar, imezindua
ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha
ugonjwa wa malaria unatokomezwa Zanzibar.
Akizindua mpango huo, Waziri wa Wizara
hiyo, Juma Duni Haji alisema kukamilika kwa ugawaji wa vyandarua hivyo kunaweza
kutokomeza moja kwa moja ugonjwa wa malaria ambao kwa Zanzibar upo chini ya
asilimia moja.
Alisema licha ya maambukizi kuwa chini
ya asilimia moja, lakini mikakati ya wizara ni kuhakikisha ugonjwa huo unabaki
kuwa historia katika Visiwa vya Zanzibar.
“Kwa kweli hadi sasa maambukizi yapo
chini ya asilimia moja, lakini mipango yetu ni kuhakikisha malaria yanabaki
kuwa historia nchi hii, ndiyo maana tunaandaa kila mkakati kufikia lengo hilo,”
alisema Duni.
Alisema jumla ya vyandarua 315, 465
vinatarajiwa kugawiwa kwa wakazi wa Unguja na Pemba ambapo Unguja vitagawiwa
vyandarua 221,803. Pemba watapata vyandarua 78,637.
Amewataja watakaonufaika na vyandarua
hivyo kuwa ni wajawazito, walemavu, wajane na waliofikwa na majanga
yanayosababisha kukosa uwezo wa kununua vyandarua.
Kwa upande wa Msaidizi Meneja wa
Kitengo cha Kupambana na Malaria Zanzibar, Mwinyi Mselem alisema pamoja na
kutoa vyandarua hivyo, kitengo chake pia kinaendelea na upigaji dawa kwa ajili
ya kuua mazalio ya mbu wa malaria.
No comments:
Post a Comment