LOWASSA ATAKA VIONGOZI WANAOUZA ARDHI WANG'OLEWE



Wananchi wa Jimbo la Monduli wilayani Monduli mkoani Arusha wametakiwa kuwang’oa madarakani viongozi wa vijiji wanaoshiriki kinyume na utaratibu kuuza ardhi bila ya kufuata utaratibu kwa kuendekeza zawadi ya bia na nyama choma.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa mara baada ya kuzindua bwawa la maji la Leken lililopo Kijiji cha Selela, Kata ya Selela wilayani Monduli lililobomoka kutokana na mafuriko ya Novemba mwaka 2011 na ukarabati wake kugharimu zaidi ya Sh bilioni 1.1.
Alisema viongozi wa vijiji wanaongoza kwa kuuza ardhi katika Wilaya ya Monduli na kibaya zaidi ardhi hiyo huuzwa kwa wageni kutoka nje ya nchi, wakati mwingine kwa kuhongwa bia na nyama choma.
Alisema wakati umefika kwa wananchi kuwang'oa viongozi wa namna hiyo kwani wanaweza kuingiza jamii ya Monduli katika matatizo makubwa kwa uroho wao binafsi kwani ni aibu kiongozi kwa kijiji kuhongwa bia na nyama choma halafu unatoa ardhi kubwa bila ya kuangalia athari ya baadaye.
Lowassa alisema mkutano mkuu wa kijiji tu ndio wenye mamlaka ya kuuza ardhi kupitia kikao halali na sio kiongozi binafsi hivyo aliwataka wananchi kuwapigia kura ya hapana viongozi wenye kushiriki kuuza ardhi kiholela kwa maslahi yao binafsi.
Alisema kasi ya kuuza ardhi ni kubwa sana hivyo ni lazima kwa kila mkazi wa Wilaya ya Monduli kuwa macho na hilo kwani hali hiyo ikiendelea kutafanya watoto wa Monduli kuwa wakimbizi katika maeneo mengine kitu ambacho ni hatari.
Lowassa ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu alisema watu wanaongezeka, lakini ardhi haiongezeki hivyo aliwaasa viongozi wa vijiji jimboni mwake kuacha kuuza ardhi kwa bakshishi ndogo kwani vizazi vijavyo vinaweza kutaabika. 
Akizungumzia maji,Lowassa aliwataka wakazi wa Kijiji cha Selela kulilinda bwawa hilo kama mboni ya jicho kwani bwawa hilo lenye uwezo wa kuhifadhi maji  yenye lita za ujazo 392,040,000 lina uwezo wa kuhifadhi maji kwa zaidi ya miaka mitatu hivyo ni jukumu la kila mtu kufuata utaratibu wa kulilinda.
Lowassa alisema alipopata ubunge mwaka 1995 tatizo kubwa katika Jimbo la Monduli lilikuwa maji pale Monduli mjini na vijijini ilikuwa tatizo kubwa na wazee wa kijiji cha Selela ndio waliokuwa wakimpa nguvu ya kuwa Mungu atamsaidia na tatizo hilo litafika mwisho na ndio maana kwa sasa Monduli ina maji hadi Kijiji cha Selela chenye wakazi 26,671.
Alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kupeleka fedha za ukarabati mabwawa 6 katika Jimbo la Monduli kiasi cha Sh bilioni 3 likiwemo bwawa la Leken na aliwataka wakazi wa mabwawa hayo kumuenzi Rais kwa kuyatunza kwa faida yao na mifugo.
Alisema bajeti ya Wizara ya Maji kwa nchi nzima inaonesha kuwa maji yamefika katika maeneo kwa asilimia 50 lakini katika Wilaya ya Monduli kwa sasa peke yake maji yameshafika kwa asilimia 60 hiyo ni jitihada nzuri na inapaswa kupongezwa. 

No comments: