Serikali
ya Tanzania imetoa uraia kwa wakimbizi 1,541 wa Somalia waliokuwa wanaishi
katika Makazi ya Chogo, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Watu hao waliikimbia Somalia mwaka 1990
baada ya kuibuka kwa vita nchini mwao ambapo 3,000 kati yao walikimbia Tanzania
walikopokelewa na kuhifadhiwa katika Kambi ya Mkuyu iliyopo mkoani Tanga ambapo
walikuwa wakipata msaada kutoka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa (UNHCR).
Akizungumza jana baada ya kuwapa vyeti
vya uraia wakimbizi hao ambao kwasasa ni raia halali wa Tanzania, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema wakimbizi hao walihamishwa na
Serikali mwaka 2003 kutoka Kambi ya Mkuyu kuja katika makazi ya Chogo ili
wapatiwe mashamba kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo ili waweze
kujitegemea.
“Nachukua nafasi hii kuwapongeza wote
waliopewa uraia wa Tanzania, wajisikie kuwa wao ni raia huru sawa na Watanzania
wengine. Hata hivyo nawasihi muwe waadilifu na watiifu kwa sheria zote za
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Chikawe.
Chikawe pia alitoa pongezi kwa UNHCR
kwa kujenga miundombinu muhimu katika makazi hayo ya Chogo na pia kuwawezesha
wakimbizi hao kuishi maisha ya kujitegemea kabla hata ya kuwa raia.
Hata hivyo, Waziri Chikawe aliwataka
wakimbizi 150 katika makazi hayo ya Chogo ambao hawakuomba kuwa raia wa
Tanzania kwa nia ya kurudi nchini Somalia pale hali ya amani itakapopatikana
wanapaswa kuendelea kutii sheria za nchi zinazotawala hifadhi ya ukimbizi
nchini.
Aidha, Mwakilishi Mkazi wa UNHCR, Joyce
Mends-Cole katika hafla hiyo aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa uraia
wakimbizi hao na Shirika lake litaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa
wakimbizi waliobaki katika makazi hayo pamoja na sehemu nyingine nchini.
Hafla hiyo ya ugawaji wa vyeti vya
uraia ilihudhuriwa na maofisa wa Idara ya Wakimbizi na Uhamiaji zilizopo Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Serikali ya
Kijiji cha Chogo na maofisa wa UNHCR.
No comments:
Post a Comment