WENYE DALADALA DAR WAHOFIA MABASI YA KASI



Wamiliki wa daladala katika Jiji la Dar es Salaam wameonesha hofu ya kutupwa nje ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) wakati wakielekea katika mchakato wa kuingia katika ushindani wa zabuni itakayotangazwa kimataifa.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi amewataka kujiamini na kujipanga, akisisitiza hakuna kisichowezekana.
Hofu ya wamiliki hao ilibainika wakati wa mkutano wa majadiliano ya wamiliki wa daladala, wakavyoweza kutambua fursa za uwekezaji kwenye mfumo wa DART, uliofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali usafirishaji.
Wamiliki hao wanahofu  kushindwa katika zabuni ya kuendesha mradi huo kwa kile wanachoeleza kutokuwa na mtaji mkubwa na uzoefu vitu ambavyo ni kigezo kikubwa katika zabuni ya mradi huo.
Walihoji inakuwaje zabuni inatangazwa wakati wao wapo na  wamefanya kazi miaka mingi ya kutoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam wakati mazingira ambayo si rafiki ikiwa ni pamoja na kuwa na miundombinu mibovu na kutaka zabuni isitangazwe kimataifa.
Wakichangia kwa nyakati tofauti wamiliki hao waliitaka Serikali kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kushiriki katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwafanya kuwa waendeshaji wakuu.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), Sabri Mabrouk alisema tayari wamiliki hao wameanzisha kampuni inayoitwa Mzizima Daladala Express, lakini wana hofu iwapo watapata nafasi ya kushiriki uendeshaji wa mradi huo.
Mabrouk alisema mashaka yao ni kuwa wanahisi kutengwa katika mradi huo kutokana na hatua ya kuambiwa daladala zao zitaondolewa na kwenda kwenye barabara za pembezoni wakati miaka yote wamekuwa wakitumia barabara hizo katika mazingira ambayo si rafiki.
“Hatuna tatizo na mradi lakini siasa nyingi imekuwa ikitumika hapa, tunaambiwa daladala zetu ziende katika barabara za pembezoni wakati barabara hizo ni mbovu…miaka yote tumetumia barabara hizi leo miundombinu inaboreshwa ndio tunaambiwa tuhame,” alisema.
Ruth Majura alisema wamiliki wa daladala, wameanzisha kampuni, lakini changamoto inayowakabili ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuandaa mpango wa kibiashara utakaowawezesha kuingia katika ushindani wa zabuni ya mradi huo.
Kwa upande wake, Gwamaka Nsekela alisema wamiliki wa daladala wana nafasi finyu ya kuingia katika tenda hiyo ya kimataifa na kuhoji iwapo kweli serikali ilikuwa na nia wamiliki hao wazawa kushiriki katika mradi huo mkubwa.
Katibu mstaafu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), Mujengi Gwao akichangia katika mkutano huo, alisema wakati Serikali inaanza mradi huo, iliahidi kuwabeba wazawa na kuitaka Serikali iwasaidie wamiliki wa daladala kwa hali na mali ili waweze kushiriki kikamilifu katika mradi huo.
Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo akijibu hoja za wadau hao alisema zabuni hiyo haijaletwa ili kuwaondoa wamiliki wa daladala, bali ni utaratibu uliowekwa kuhakikisha anapatikana mtu atakayeweza kuendesha mradi huo kwa ufanisi.
Aliwataka wamiliki hao kuimarisha, kuijengea nguvu na uwezo kampuni yao ili waweze kuingia katika ushindani wa zabuni na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria na Taratibu Serikali haiwezi kutoa upendeleo wowote kwa wazawa hao.
Mshauri Mwezeshaji wa DART, Felix Mlaki aliwataka wamiliki hao kufanya juhudi kutafuta mtaji wa kutosha katika kampuni yao kwa kile alichoeleza kuwa kigezo kimojawapo katika zabuni hiyo ni mtaji na uzoefu na kwamba Juni 3 na Juni 4, mwaka huu kutakuwa na mkutano wa wadau wa ndani na nje kujadili namna ya kushiriki katika zabuni.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymon Mushi aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alisema hakuna lisilowezekana na kuwataka wamiliki hao kujipanga, kuimarisha kampuni yao ili iweze kuingia kwenye ushindani.

No comments: