MWIMBAJI AMINA NGALUMA 'JAPANESE' AZIKWA

Mwanamuziki Amina Ngaluma ‘Japanese’ aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand amezikwa leo jioni kwenye makaburi ya Machimbo Mnarani Dar es Salaam.
Mwili wa Ngaluma uliwasili nchini jana jioni kutoka Thailand alipokuwa akifanya kazi ya muziki na bendi ya Jambo Survivor.
Wanamuziki mbalimbali na  wadau walikusanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuupokea mwili wa Ngaluma aliyefariki wiki iliyopita kwa shinikizo la damu kabla ya kujumuika na familia yake jana kwa ajili ya maziko.
Akizungumza baada ya maziko hayo, mume wa Ngaluma, Rashid Sumuni aliwashukuru wanamuziki, wadau wa muziki na vyombo vya habari.
“Nawashukuru wote kwa ushirikiano wenu tangu kupata taarifa za msiba wa marehemu mke wangu, asanteni kwani tumemhifadhi salama  mke wangu, tumuombee dua,” alisema.
Wakati wa uhai wake, Ngaluma  alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’,  Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili,  Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’.

No comments: