Wadau wa haki jinai mkoani Kagera
wametakiwa kuzingatia haki za akinamama na watoto, ambao ni waathirika wa vitendo vya kikatili ili
waweze kupata haki zao za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Jaji wa
Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Peragia Khadai wakati wa kikao cha siku moja
cha wadau hao kutoka wilaya zote za mkoa
huo kwa lengo la kutekeleza miongozo, kanuni na maelekezo ya viongozi wao.
“Sio kwamba napendelea kundi hilo la
akinamama ambao huathirika na vitendo vya kikatili, bali tuzingatie udhaifu wa
kundi hili kwani wamekuwa wakipata taabu wanapofika mahakamani,
hawana uzoefu katika kuweka mawakili wa kuwatetea hivyo tuwasaidie na
kuwasikiliza wasije kuathirika mara ya pili ,” alisema.
Alisema takwimu zinaonesha katika Mkoa
wa Kagera bado yapo mashauri mengi ya jinai, ambayo ni ya muda mrefu kuanzia mwaka 2009.
Alisema baadhi ya watuhumiwa wapo
mahabusu katika magereza ya mkoa muda mrefu,
kwa hiyo ni vema suala hili likapatiwa ufumbuzi ni kwa jinsi gani
linaweza kumalizika.
Aliwataka wapelelezi wakiongozwa na
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa
Mkoa, Henry Mwaibambe kufanya kazi yao kwa weledi kwa kutumia vifungu vya
sheria, kanuni na miongozo mbalimbali na kuzingatia masuala ya haki za binadamu
katika hatua zote za upelelezi.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali,
Sakina Sindah alisema wamekuwa wakijikuta na masuala mengi juu ya utekelezaji
wa sheria mpya ya watoto, hasa wale wanaokabiliwa na tuhuma za jinai katika
vituo vya polisi.
Alisema kupitia wadau hao, wataweza
kulitatua na kulipatia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment