WAMILIKI WA MABASI WAJIFUNZA FURSA NDANI YA BRT



Wamiliki wa mabasi ya abiria Dar es Salaam na wadau wengine watakutana jijini humo kujifunza fursa na kufahamu namna ya kushiriki katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) unaotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.
Kwa mujibu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Karimjee na utatumika pia kuelezea mkutano mwingine wa kimataifa utakaofanyika Juni 3 na 4 kujadili kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo aliwaambia waandishi wa habari jijini humo jana kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki atakuwa mgeni rasmi katika mkutano huo muhimu.
“Mkutano huo unalenga kuwaelezea wamiliki wa mabasi ya abiria maarufu kama daladala na wale wa UDA fursa za mradi wa mabasi yaendayo haraka na jinsi wanavyoweza kuwa wadau, wataelezewa faida na fursa za mradi huo mpya na jinsi wanavyoweza kushiriki,” alisema Mlambo.
Mkutano huu pia unalenga kupata maoni ya wadau hao wa usafiri na kuyatumia kama mchango katika mkutano wa kimataifa wa Juni. Aliwataka wamiliki hao wa mabasi ya abiria kuhudhuria kwa wingi na kushiriki kikamilifu.
Aprili mwaka huu, DART ilikamilisha zoezi la kusajili mabasi ya daladala yanayopita katika barabara ya Morogoro na yake yanayokatiza katika njia hiyo.
Hatua hiyo ilikuwa moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo wa mabasi yaendayo haraka na hivi sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza.
Awamu hiyo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.
Jumla ya njia 64 jijini Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo unaolenga kupunguza tatizo sugu la msongamano wa magari jijini humo.

No comments: