MABASI YALIPA 65,000/- KUPULIZA DAWA YA HOMA YA DENGUE



Mabasi yaendayo mikoani yanalipa Sh 65,000 kwa ajili ya kupuliza dawa ndani ya magari hayo ikiwa ni hatua ya kupambana na ugonjwa wa dengue nchini. Imeelezwa.
Hatua hiyo imetokana na makubaliano ya wamiliki wa mabasi hayo na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kudhibiti ugonjwa huo kuenea katika mikoa mingine yanakofanya safari zake.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe alisema hayo jana akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM) aliyetaka kujua kwa nini upulizaji wa dawa katika mabasi, unatozwa gharama kubwa na mikakati ya dharura kukabiliana na ugonjwa huo.
Dk Kebwe alisema malipo hayo ni makubaliano ya wamiliki wa magari, kutokana na uzalendo wa nchi na kukabiliana na ugonjwa huo, hivyo hakuna mmiliki anayeshindwa kulipa fedha hizo.
Alisema mipango ya dharura, kukabiliana na ugonjwa huo ni pamoja na kuvipatia vitendea kazi vituo vyote vya afya nchini, kuweza kubaini maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema pia vipo vipimo vingine vinatarajia kuwasili nchini kupitia Bohari ya Madawa nchini (MSD) na vitaongeza upatikanaji wake pale vinapohitajika.

No comments: