HUDUMA ZA UZAZI WA MPANGO ZATENGEWA SHILINGI BILIONI 3



Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetenga kiasi cha Sh bilioni 3 katika bajeti ya fedha ya mwaka 2014/15 kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe S. Kebwe wakati akizindua upya kampeni ya Nyota ya Kijani kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Michezo wa Nyamagana.
Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), wametoa Sh bilioni 6.4 ikiwa ni pamoja na vifaa ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya huduma ya uzazi wa mpango.
Alisema kiwango cha utumiaji wa uzazi wa mpango kipo juu katika nchi zilizoendelea, ambapo ni asilimia 72.4.
Alisema Tanzania kiwango cha utumiaji, bado kipo chini, ikiwa ni asilimia 27 hivyo Watanzania wanapaswa kwenda sambamba na maelekezo ya dunia ili wasipitwe na wakati.
Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri huyo alitoa wito kwa wadau wote, kuungana pamoja katika kuongeza kasi ya upatikanaji na utumiaji wa huduma za uzazi wa mpango.
Alisema imani potofu imechangia utekelezaji wa huduma za uzazi wa mpango kwenda polepole, hasa kwa upande wa wanaume ambao ushiriki wao umekuwa mdogo kwa kuhofia nguvu za kiume kupungua, imani ambayo siyo ya kweli.
“Tumemuona ndugu yetu Mayunga ametoa ushuhuda wake mbele yetu hajazungumzia nguvu za kiume kumpungua tangu afanyiwe, ushuhuda
uliotolewa ni elimu tosha kuliko kwenye majukwaa,” alisema Naibu Waziri Kebwe.
Alisema ukosefu wa uzazi wa mpango katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, unachangia kurudisha nyuma takwimu za kitaifa, ambapo kwa sasa ni asilimia 12 wakati Kanda ya Kaskazini inafikia asilimia 50.
Alisema uzinduzi mpya wa kampeni ya Nyota ya Kijani, yenye kaulimbiu ya ‘Fuata nyota ya kijani upate mafanikio’ ni njia pekee ya kuondokana na imani potofu miongoni mwa jamii.
Alisema Mkoa wa Mwanza una vituo 363 vinavyotoa huduma za afya za mama na mtoto, vikiwemo vituo 72 vinavyotoa huduma ya uzazi wa mpango.
Alisema uzinduzi unaofanyika, utakuwa chachu ya mabadiliko na ari mpya katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa dawa za uzazi wa mpango za kutosha na kwa wakati na
kupiga vita na kuondoa dhana potofu kuhusu njia za kisasa za uzazi wa mpango.

No comments: