NDERUMAKI ATEULIWA KUWA MHARIRI MTENDAJI WA TSN



Rais Jakaya Kikwete, amemteua Gabriel Nderumaki, kuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), wachapishaji wa magazeti ya Habari Leo, Habari Leo Jumapili, Spoti Leo, Daily News na Sunday News.
Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, uteuzi huo umeanza Mei 19, 2014.
Kabla ya uteuzi huo, Nderumaki alikuwa Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo tangu Desemba 2012. Nafasi zingine alizowahi kushika ni pamoja na Mhariri wa Michezo, Mwandishi Mkuu, Mhariri wa Habari na  Mhariri wa Biashara wa gazeti la Daily News.
Nderumaki ambaye amekuwa katika fani ya habari tangu 1994, ana Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine aliyoipata mwaka 2013.
Pia ana Shahada ya kwanza Uhusiano wa Umma na Matangazo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Stashahada ya Juu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma kutoka iliyokuwa Shule ya Habari (TSJ) na Cheti cha Ualimu kutoka Chuo cha Ualimu Kinampanda, Singida.
Nderumaki pia amewahi kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja ya kijeshi katika Kambi ya Msange, Tabora na kuhudhuria mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

No comments: