MAKTABA KUU WAELEMEWA NA MAHITAJI YA TAARIFA KWA TEHAMA



Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (Bohumata) imesema mahitaji ya taarifa yanayotolewa kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa jamii yameongezeka maradufu hali inayowafanya washindwe kutoa huduma nzuri.
Aidha, Bodi hiyo inashindwa kugharimia huduma hizo kutokana na uwezo wa kifedha kuwa mdogo.
Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Bohumata, Comfort Komba alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kuwepo kwa ukosefu wa fedha zipo juhudi za kuendelea kutoa huduma ya TEHAMA katika vituo vingine.
“Kwa sasa huduma hii ipo katika Maktaba ya hapa Dar es Salaam lakini tunajitahidi kupeleka katika vituo vingine ili kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya nchi kwa kupata taarifa sahihi na kwa wakati,” alisema Komba.
Akifafanua kuhusu mfumo wa Tehama, Komba alisema ni katalogi ya kielektroniki inayowezesha kutoa mchango mkubwa katika kusaidia juhudi za serikali za kuelimisha jamii kwa kupatikana kwa habari kutoka katika vitabu, magazeti, ramani na picha kwa haraka zaidi.
“Mfumo huu una uwezo wa kutunza kumbukumbu nyingi kwa kutumia nafasi ndogo katika maktaba kwani habari huwa katika mfumo wa kielektroniki, pia unahamasisha matumizi ya kielektroniki, kuhabarishana na kuhamasisha matumizi ya habari kwa jamii,” alisema.
Alisema kwa sasa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi wa Nyaraka (Slads) cha Bagamoyo kimeongeza udahili wa wanafunzi mpaka kufikia 1,093.  Alisema idadi hiyo imekuwa kubwa kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa wanataaluma wa ukutubi na uhifadhi nyaraka kwenye shule za serikali na za watu binafsi, vyuo, taasisi na ofisi mbalimbali nchini.

No comments: