WALIMU, WANAFUNZI NA SHULE BORA WAJAZWA MANOTISerikali jana ilimwaga mamilioni ya fedha kwa wanafunzi, walimu, shule, halmashauri na mikoa iliyofanya vizuri katika elimu miongoni mwake ikiwa ni kitita cha Sh milioni tatu kilichotolewa kwa shule 60 kila moja kwa ajili ya walimu walioleta maendeleo. 
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal ndiye aliyekabidhi tuzo hizo mjini hapa kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu Kitaifa.
Aidha katika maadhimisho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia kwa Waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa imesema inaandaa uchangiaji wa kitaifa wa madawati kwa ajili ya kukabili uhaba wa vifaa hivyo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya elimu. 
Katika maadhimisho hayo ambayo shule 3,217 zilizawadiwa, ikiwa ni motisha chini ya mikakati tisa iliyoibuliwa na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Dk Bilal aliasa shule zilizopata zawadi kuhakikisha zinaendeleza bidii zidumu kushinda. 
Dk Bilal ambaye alitaka mikoa mingine kuiga mfano wa Mkoa wa Kagera ambao ulitajwa mara kwa mara kwa kuwa na shule zilizofanya vizuri, alitaka shule ambazo hazikupata zawadi pia kujifunza kwa wenzao. 
Tuzo zilizotolewa na Makamu wa Rais ni kwa wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana. 
Shule 60 zilizoonesha maendeleo mazuri zimepatiwa Sh milioni tatu kwa kila shule. Fedha hizo zimeelezwa kwamba ni mahususi kwa walimu wa shule hizo waliochangia kuleta maendeleo. 
Tuzo zimekwenda pia kwa shule 10 zilizofanya vizuri ambazo kati yake, tano ni za elimu ya msingi na zilizobaki ni za sekondari. 
Wakati huohuo, Halmashauri ya Mbinga, mkoani Ruvuma pamoja na Mkoa wa Tanga wamepewa tuzo kwa kufanya vizuri kitaaluma.  Wengine waliopewa tuzo ni shule 10 za msingi na sekondari  zilizoonesha maendeleo ya juu. 
Katika maadhimisho hayo, pia zawadi zilikabidhiwa kwa washindi 13 wa uandishi wa insha ambapo washindi 10 ni uandishi wa insha za mashindano ya Afrika Mashariki. Washindi watatu ni wa insha za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). 
Kwa mujibu wa Dk Kawambwa, utaratibu wa tuzo kwa wanafunzi, walimu, shule, halmashauri na mikoa unalenga kuhamasisha wanafunzi, walimu na jamii kuongeza bidii kuleta matokeo bora zaidi. 
Akizungumzia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, alisema miezi 11 tangu utekelezaji wa Mpango huo, sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa.  Pia ufaulu wa elimu ya msingi na elimu ya sekondari umeongezeka kutoka asilimia 31 na 43 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 50.6 na asilimia 58.3 mwaka jana.

No comments: