SERIKALI YAKERWA NA VITENDO VYA UCHOMAJI MAKANISA



Serikali imetoa tamko juu ya mfululizo wa vitendo vya uchomaji makanisa vilivyoibuka hivi karibuni na kusema  imeagiza dola ikaze uzi kukabili wimbi hilo. 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema juzi bungeni wakati akihitimisha michango ya wabunge kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 ya ofisi yake iliyopitishwa jana. 
Alisema kati ya Februari 6 na Mei 5, mwaka huu, jumla ya makanisa matano yamechomwa moto au kukumbwa na milipuko ya mabomu katika maeneo mbalimbali nchini. 
Alitaja makanisa hayo na maeneo yalikochomwa ni Living Water la Bukoba lililochomwa Februari 6, Kanisa la Pentekoste la Kihonda Morogoro lililochomwa Machi 3 na kanisa moja Zanzibar lililokumbwa na mlipuko Februari 19.
Mengine ni Kanisa la Pentekoste la Mafia lililochomwa Mei 3, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la mjini Mwanza lililokumbwa na mlipuko wa bomu Mei 5 mwaka huu. 
“Trend (mwenendo) hii si nzuri. Nataka niombe radhi wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanajikuta kwenye purukushani za namna hii,” alisema. 
Alisihi Watanzania kwamba hali hii si nzuri. Alisema nchi hii haikuzoea hali ya milipuko, lakini imeanza kujitokeza hivi karibuni. 
“Tulichofanya tumeviambia vyombo vya dola vikaze uzi zaidi kidogo kujaribu kuona chanzo ni nini na tunaikabili namna gani. Vinginevyo vitatupa tabu sana huko tunakokwenda,” alisema Pinda. 

No comments: