WAKIMBIZI 32,000 NCHINI KUHAMISHIWA MAREKANIWakimbizi wenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi wapatao 32,000 walioko nchini, wanatarajiwa kuhamishiwa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitoa taarifa hiyo jana bungeni mjini hapa, kwamba huo ni mpango maalumu unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.
Alisema unatekelezwa katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani baada ya serikali kusaini mkataba na mashirika ya Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR)  na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
“Katika mwaka 2014/2015, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani itaanza kutekeleza Mpango Maalumu wa kuwahamishia nchini Marekani wakimbizi wenye asili ya DRC na Burundi wapatao 32,000…,” alisema.
Aidha, alisema katika mwaka 2013/2014 serikali kupitia wizara hiyo, ilitoa uraia kwa wakimbizi wa Kisomali 1,514 wenye asili ya kibantu waliokuwa wakiishi katika makazi ya Chogo wilayani Handeni mkoani Tanga.
Kwa kuzingatia uamuzi huo, makazi hayo yamefungwa rasmi Februari mwaka huu na wakimbizi wapatao 150 ambao wamebaki katika eneo hilo wataendelea kuishi hapo kwa mujibu wa sheria ya wakimbizi ya mwaka 1998.
Waziri alisema hadi Machi 31 mwaka huu, idadi ya wakimbizi ambao wanahifadhiwa nchini ilikuwa 97,783 ikilinganishwa na wakimbizi 101,183 waliokuwepo nchini Machi 31 mwaka jana.
Wakati huo huo, waziri alisema katika mwaka 2014/15, serikali itaendelea na jitihada za kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la wakimbizi kwa kuwarejesha nyumbani ambao hali ya amani na usalama itakuwa imerejea kwenye nchi zao za asili.
Aidha taratibu zinakamilishwa kuhusu hatma ya wakimbizi wa Burundi wapatao 162,156 wa mwaka 1972.

No comments: