MABASI, HOTELI KUPULIZIWA DAWA KUJIKINGA NA HOMA YA DENGUEMkoa wa Dar es Salaam umeagiza kupulizia dawa za kuua mazalio ya mbu katika mabasi yanayoenda nje ya Dar es Salaam, katika hoteli, shule na vyuo, masoko na majengo yote ya taasisi za serikali na binafsi ili kupambana na ugonjwa wa dengue.
Aidha, imeelezwa kuwa katika mkoa huo wagonjwa walioathirika mpaka juzi ni 494 waliogundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa dengue ambapo 389 wilaya ya Kinondoni,73 Ilala na 32 Temeke.
Alisema  kati ya wagonjwa hao waliolazwa mapaka sasa ni 11 ambapo sita wako hospitali ya Temeke, wanne Amana na mmoja Burhani huku vifo vilivyothibitika vikiwa vitatu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema hayo jana wakati akielezea hali ya ugonjwa huo katika mkoa na hatua zilizochukuliwa, ambapo alibainisha upuliziaji wa dawa, siyo lazima kwa  maeneo yote.
Aliwataka maofisa afya, kuhakikisha wanakagua maeneo hayo na kuwachukulia hatua wasiofanya hivyo.
Aidha, aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kupanga ratiba itakayohakikisha mabasi yanayotoka katika kituo cha Ubungo, yanapuliziwa dawa za kuua vimelea hivyo ili mbu hao, wasikae katika mizigo au ndani na kusababisha kusambaza nchi nzima.
“Katika kituo kuna mabasi zaidi ya 600, hivyo lazima wapangiwe ratiba na wamiliki wameishakubali kugharamia upuliziaji huo hivyo atakayekaidi tutamfungia kutoa huduma ya usafirishaji,” alisema.
Alisema serikali inapuliza dawa katika shule na vyuo vyake na aliwataka wamiliki kufanya hivyo ili kuwakinga watoto, wanaoshinda katika mazingira hayo, kutokana na kuwa mbu wa ugonjwa huo anauma mchana.
“Tumeandika barua, kwa wakuu wa shule na wamiliki wa shule binafsi kusafisha mazingira ya shule na kupuliza dawa za kuua mbu, na tayari ofisi za umma, shule, hospitali na vituo vya afaya 20 vimepulizwa dawa,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa nguo zinazofunika sehemu za mwili kama miguu ,mikono au kupaka dawa ya kufukuza mbu kama ni lazima kuwa maeneo hayo.
Katika kukabiliana na ugonjwa huo, alisema halmashauri zimetenga Sh milioni 218  kwa ajili ya vifaa, elimu kwa jamii na kupulizia dawa, huku Temeke ikiongoza kwa kutenga Sh milioni 224, ikifuatiwa na Kinondoni iliyotenga sh milioni 150 na Ilala imetenga Sh milioni 32.

No comments: