WABUNGE WAPINGA SHILINGI 500 KWA MILO MITATU YA WAFUNGWA



Bajeti ndogo ya chakula cha wafungwa ya Sh 500 kwa siku, maslahi madogo pamoja na makazi duni kwa askari walio chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, vimevaliwa njuga na wabunge ambao wametaka Serikali iiongezee wizara fedha katika bajeti ijayo. 
Wizara hiyo inayohudumia jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji  kupitia kwa Waziri wake, Mathias Chikawe, jana iliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh 881,740,291,800 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kiwango hicho kimetajwa kuwa ni kidogo ikilinganishwa na majukumu ya wizara hiyo.
Wabunge mbalimbali waliochangia, ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Anna Abdallah, walieleza kusikitishwa na kitendo cha wafungwa kupangiwa Sh 500 kwa siku kwa kusema kibinadamu si sahihi kumlisha mtu kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya milo mitatu.
Licha ya kusisitiza posho ya wafungwa iongezwe hadi Sh 3,000 kwa siku, wabunge hao hasa kamati, pia walisisitiza serikali iongeze posho ya chakula kwa askari wote chini ya wizara hiyo kutoka Sh 5,000 hadi Sh 7,500 kwa siku.
Akisoma taarifa ya kamati, Hilda Ngoye alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2013/14 pamoja na maoni kuhusu makadirio na mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Kwa mujibu wa Ngoye, maelezo ya serikali ni kwamba katika mwaka wa fedha 2013/14,  kiwango cha posho kwa wafungwa kilibaki kile kile cha Sh 500 kwa siku kutokana na ufinyu wa bajeti. “Na kwamba hali itakuwa vivyo hivyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015,” alisema Ngoye.
Pia kwa upande wa posho ya askari, alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014, kamati ilishauri posho hiyo iongezwe lakini haikuongezwa.
“Kamati inazidi kuisisitiza serikali kuwa Sh 5,000 kwa siku ni ndogo kwa kuzingatia gharama halisi ya chakula na aina ya kazi wanazofanya,” alisema.
Hata hivyo katika taarifa hiyo ya bunge, imeelezwa maelezo yaliyotolewa na serikali juu ya suala hilo ni kwamba wizara imekamilisha taratibu za kuomba nyongeza hiyo ya posho  kwa askari na kuwasilisha mapendekezo katika Tume ya Rais ya Menejimenti ya  Utumishi wa Umma kwa hatua zaidi kabla ya kuwasilishwa Hazna.
Akichangia, Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema alisema haiwezekani polisi akaishi kwa Sh 5,000 ya chakula kwa siku. Alihoji kama wanafunzi wa vyuo vikuu  wanapangiwa posho ya Sh 10,000 kwa siku, iweje polisi apewe Sh 5,000 kwa siku.
Mrema alikosoa pia  hatua ya wafungwa kupangiwa bajeti ya Sh 500 kwa siku na kusema huo ni ukiukaji wa haki za binadamu. 
“Mfungwa asihukumiwe kwa kunyimwa chakula,” alisema na kushauri kamati ya ulinzi kukutana leo na Kamati ya Bajeti kubadilisha viwango hivyo vya posho.
Mbunge wa  Konde, Khatib Said Haji (CUF) alihoji  vigezo vilivyozingatiwa kupangia wafungwa Sh 500 za chakula kwa siku. Alisema kuridhia wafungwa waendelee  kupangiwa bajeti hii ni kutowatendea haki na ni laana kwa Mungu.
Mbunge wa Kuteuliwa, Anna Abdallah alitaka wabunge kuhakikisha wanaibana  Serikali wizara hiyo ya Mambo ya Ndani ya Nchi iongezwe fedha imudu kutekeleza mahitaji yake, ikiwemo kuboresha hali ya maisha ya askari.
Katika majumuisho yake, Chikawe alikubaliana na hoja nyingi za wabunge, ikiwa ni pamoja na bajeti ya mlo wa wafungwa, akisema wameomba Hazina kiwango kipande na kufikia Sh 3,000 kwa siku, na kama ikishindikana, kiwe Sh 1,500 kwa siku kama ilivyokubaliwa mwaka wa fedha uliopita. Kwa upande wa posho za askari, alisema wameomba kiwango kipandishwe na kufikia Sh 8,000 kutoka Sh 5,000 ya sasa.

No comments: