WAJENZI WAZALENDO WASHAURIWA KUWEKEZA MJI MPYA KIGAMBONI



Kampuni binafsi za kitanzania zimetakiwa kuwekeza katika ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni.
Mwito huo ulitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM).
Katika swali lake Mtemvu alitaka kujua Wizara hiyo imewashirikishaje wawekezaji wa ndani ikiwemo mifuko ya hifadhi za jamii na kampuni za kitanzania.
Simbachawene alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi.
“Serikali imedhamiria kujenga Mji Mpya wa Kigamboni ili kuwa mji wa kisasa ambao utakuwa kitovu cha kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema.
Alisema baadhi ya mashirika ya kiserikali kama Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) yameanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi mpya wa Kigamboni kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara ndani ya eneo la mradi.
“Mwaka 2007 Serikali iliandaa Mpango Kabambe wa kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji na Sheria ya Utwaaji Ardhi.
“Mpango huu umeainisha maeneo ya matumizi makubwa ya ardhi ikiwemo viwanda, makazi, taasisi za elimu, biashara, utalii na miundombinu,” alisema Simbachawene.
Alisema katika mwaka 2013/14 Serikali imeunda Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni (KDA) kwa lengo la kusimamia na kuratibu uendelezaji wa Mji wa Kigamboni.

No comments: