MAHABUSU ZA WATOTO KUJENGWA KILA MKOA



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima amesema Serikali ina mpango wa kujenga mahabusu za watoto katika kila mkoa nchini.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Omar Juma (CUF).
Katika swali lake mbunge huyo alitaka kujua lini Serikali itajenga mahabusu za watoto ili kuwapunguzia udhalilishaji na manyanyaso wanapochanganywa na watu wazima.
Silima alisema kwa kuanza mahabusu hizo zitajengwa mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha na Morogoro.
Alisema ufinyu wa bajeti kwa Wizara ndio kikwazo cha utekelezaji wa mpango huo.
Alisema lengo la Tanzania ni kuwa na mfumo mahususi wa kushughulikia watoto wenye mgogoro wa sheria kwenye mahakama za watoto, mahabusu na shule za maadili ya watoto watukutu.
Alisema kwa sasa nchi nzima ina mahabusu sita za watoto, mahakama moja na shule ya maadili moja.
Silima alisema Sheria za Kimataifa zinaelekeza watoto wenye mgogoro wa sheria wasihifadhiwe kwenye mahabusu na magereza ya watu wazima bali wawe na mfumo wao wenyewe ambao hapa nchini upo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Naibu Waziri huyo alisema kutokana na upungufu huo uliopo nchini, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), imeanzisha mradi maalumu wa kulifanyia utafiti tatizo hilo.
Alisema katika utafiti huo mapendekezo yatatolewa ili kupata suluhisho la kudumu.

No comments: