PINDA AZUNGUMZIA SAKATA LA MGOMO WA TAZARAWaziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali inalifanyia kazi suala la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ambao wamegoma ili kurejesha mawasiliano ya usafiri.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Suzan Kiwanga.
Waziri Mkuu alisema tatizo la mgomo wa wafanyakazi wa Tazara linajulikana na litashughulikiwa ili  usafiri urejee katika hali ya kawaida na kurudisha mawasiliano.
“Suala la mishahara ya wafanyakazi linafanyiwa kazi ili usafiri urejee katika hali ya kawaida,” alisema.
Aidha Waziri Mkuu amesema mvua zilizonyesha katika Mkoa wa Morogoro zilikuwa ni nyingi na moja ya athari zilitokea katika kivuko cha Kilombero.
Alisema kutokana na tatizo hilo Jeshi limeombwa kusaidia uvushaji wa wananchi wakati wa kusubiri maji kupungua.
Pia alisema kata 14 zimeathirika.
Katika swali la msingi, Kiwanga alisema mafuriko yamepelekea kata 14 za Wilaya ya Kilombelo kukosa mawasiliano huku akinamama wajawazito wanakufa kwa kukosa huduma.
“Jana (juzi), wafanyakazi wa Tazara wamegoma kwa kutolipwa mshahara wa miezi mitatu ni namna gani wanaokoa kwa kupeleka fungu maalum kwa kuboresha miundombinu Wilaya ya Kilombero na Ulanga. Je Uko tayari kusaidia Kilombero kwa fungu la maafa?” alihoji.

No comments: