Watahiniwa 24,204
wa Kidato cha Nne mwaka 2013, hadi sasa hawajawasilisha malipo ya ada zao kwa
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), ili kupatiwa matokeo yao, Bunge
limefahamishwa.
Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema hayo bungeni akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalumu, Kuruthum Mchuchuli (CUF).
Mchuchuli alitaka
kufahamu ni wanafunzi wangapi wa Kidato cha Nne ambao hawajapata matokeo yao
kwa sababu ya kutolipa ada za mitihani.
Dk Kawambwa alisema
matokeo ya Kidato cha Nne 2013 yalitangazwa Februari 21, 2014 ambapo matokeo ya
watahiniwa 31,518 kati ya 404,083 waliofanya mtihani huo yalizuiwa kwa sababu
za kutolipa ada.
“Idadi hiyo ni
sawa na asilimia 7.79 ya watahiniwa waliofanya mtihani. Matokeo ya mtahiniwa
yaliyozuiwa hufunguliwa mara moja baada ya mtahiniwa husika kulipa ada yake ya
mtihani.
“Hadi tarehe 8,
Mei 2014, jumla ya watahiniwa 7,314 wameshawasilisha ada zao na kufunguliwa
matokeo yao na hivyo idadi ya watahiniwa ambao bado hawajawasilisha malipo yao
ya ada ni 24,204,” alisema Waziri Dk Kawambwa.
Aliwahimiza
wazazi na walezi wa watahiniwa ambao matokeo yao yamezuiliwa kwa kutolipa ada
ya mtihani, kulipa ada hizo mapema ili matokeo hayo yafunguliwe na kutoa fursa
ya wanafunzi hao kuendelea na kozi mbalimbali kulingana na matokeo hayo.
No comments:
Post a Comment