HOTUBA
YA WAZIRI WA UJENZI, MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE
MAGUFULI (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO WA MAENDELEO NA
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA
KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15
A.
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, naomba kutoa hoja kwamba Bunge
lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti
ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2013/14. Aidha, lijadili na kupitisha
Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunilinda na kunipa nguvu na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako
Tukufu kuwasilisha bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2014/15. Ni
Mungu pekee aliyetulinda kipindi tulipopata ajali ya helikopta mnamo tarehe 13
Aprili, 2014 nikiwa pamoja na Viongozi wengine wa Serikali. Ninawashukuru sana kwa sala zenu.
3. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa wetu, kwa kuwa mstari wa mbele katika kutafuta
fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha, nawapongeza Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilali, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter
Pinda, Waziri Mkuu kwa namna ambavyo wamemsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia na
kuongoza shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
4. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kutoa rambirambi na
salamu za pole kwako wewe Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wabunge, familia,
ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dkt. William Mgimwa na Marehemu Saidi
Bwanamdogo, waliokuwa Wabunge wa Jimbo la Kalenga na Jimbo la Chalinze.
Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole na kumwomba Mwenyezi Mungu
aendelee kutoa faraja kwa familia na ndugu. Mwenyezi Mungu aziweke roho za
marehemu mahali pema peponi, Amina.
5. Mheshimiwa Spika, nachukua
fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Godfrey Mgimwa (Mb.) na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa
Wabunge.
6. Mheshimiwa Spika, nawapongeza
wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba (Mb.) na Makamu
Mwenyekiti Mheshimiwa Profesa Juma Athumani Kapuya (Mb.) kwa ushauri wao wenye
tija kwenye sekta ya Ujenzi. Wizara ya Ujenzi inazingatia ushauri unaotolewa na Kamati hii pamoja na Wabunge wote
katika utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, nampongeza Mhe. Felix Mkosamali (Mb) kwa
kuteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Ujenzi toka Kambi ya Upinzani.
7. Mheshimiwa Spika, ufafanuzi kuhusu Dira, Dhima, Majukumu, Malengo na
Mikakati ya Wizara Ujenzi umeainishwa katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ukurasa wa 4 - 7.
B: TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI
YA MWAKA WA FEDHA 2013/14
8. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ilipanga
kukusanya Shilingi 45,047,550.00.
Hadi kufikia Aprili, 2014 Shilingi
40,385,200.00 zilikuwa zimekusanywa (sawa na asilimia 89.65). Aidha, Wizara
ilitengewa kiasi cha Shilingi
381,205,760,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Hadi kufikia Aprili
2014, Shilingi 372,088,829,186.73 zilitolewa
na HAZINA kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (sawa na asilimia 97.61). Kati
ya fedha hizo zilizotolewa, Shilingi
18,196,824,680.00 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Wizara na
Taasisi zake, Shilingi
352,114,418,206.73 ni fedha za Mfuko wa Barabara na Shilingi 1,777,586,300.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo ya
Wizara na Taasisi zake.
9. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
iliidhinishiwa na Bunge Shilingi 845,125,979,000.00
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 448,174,599,000.00 ni fedha za
ndani na Shilingi 397,051,380,000.00 ni
fedha za nje. Fedha zilizotolewa hadi Aprili, 2014 ni Shilingi 604,405,943,800.00 ambazo zinajumuisha Shilingi 347,328,096,167.00 fedha za
ndani na Shilingi 257,077,847,633.00
fedha za nje. Kiasi cha fedha zilizotolewa ni sawa na asilimia 71.52 ya fedha iliyoidhinishwa
na Bunge kwa mwaka wa fedha 2013/14.
10.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Aprili, 2014, kwa upande wa barabara kuu, jumla ya kilomita 600.17 kati ya kilomita 495 zilizopangwa kujengwa kwa kiwango
cha lami zilikamilika na kilomita 193.5
kati ya kilomita 190.00 zilizopangwa
zilikarabatiwa kwa kiwango cha lami. Kwa
upande wa barabara za mikoa kilomita 59.25
kati ya kilomita 66.1 zilijenga kwa
kiwango cha lami na kilomita 424.5
kati ya kilomita 867.6 zilifanyiwa
ukarabati kwa kiwango cha changarawe.
11.
Mheshimiwa Spika, ujenzi
wa Madaraja manne (4) ya Kikwete katika Mto Malagarasi, Nangoo, Nanganga na
Ruhekei ulikuwa umekamilika. Aidha,
ujenzi wa madaraja makubwa 6 (Kigamboni,
Mbutu, Maligisu, Kavuu, Kilombero na Sibiti) unaendelea vizuri na usanifu wa
daraja la Ruhuhu unaendelea.
12.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Mwezi Aprili, 2014 jumla ya km 7,412
kati ya km 11,276.87 na madaraja
836 kati ya 1,272 ya barabara kuu yalifanyiwa matengenezo ya kawaida na ya muda
maalum (routine and periodic maintenance) na kwa upande wa barabara za mikoa km
14,192 kati ya 24,489.09 na madaraja 707
kati ya 1,305 yalifanyiwa
matengenezo. Ufafanuzi zaidi kuhusu
Miradi ya Ujenzi na Ukarabati wa Barabara na Madaraja umefafanuliwa zaidi
katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti Ukurasa
10 - 71.
13.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara imeendelea kutekeleza miradi ya barabara za kupunguza
msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam zenye urefu wa kilometa
109.35 na kuwezesha kukamilika kwa Barabara
ya Ubungo Bus Terminal – Mabibo – Kigogo Round About (km 6.4) na barabara ya Jet Corner – Vituka – Devis Corner (km 10.30). Aidha, Barabara ya Kigogo Round About – Bonde la
Msimbazi – Twiga/Msimbazi Jct (km 2.7); Mkandarasi anaendelea na kazi ya
kujenga kwa kiwango cha lami ambapo maendeleo ya mradi kwa ujumla yamefikia
asilimia 75.
14. Mheshimiwa Spika, barabara ya Tabata Dampo –
Kigogo (km 1.65) na Ubungo Maziwa - External (km 2.25) kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami zinaendelea.
15. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo
Haraka unahusisha ujenzi wa barabara
kutoka Kimara hadi Kivukoni (km 15.8), Magomeni hadi Morocco (km 3.4) na Fire
hadi Kariakoo km (1.7) pamoja na vituo vya mabasi 27, vituo vikubwa (depots)
vya mwisho vitatu katika maeneo ya Kimara, Ubungo na Morocco na madaraja ya
waenda kwa miguu matatu. Hadi kufikia Aprili, 2014, kazi zilizofanyika ni
asilimia 65.
Aidha, Karakana (Depot) ya Jangwani; imefikia asilimia 70 na Ujenzi
wa Kituo Kikuu cha Mabasi (Terminal) cha Kivukoni umefika asilimia 95. Pia Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi
(Terminal) cha Kariakoo kazi
zimeanza (mobilization).
16. Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Vituo
vya Mlisho (Feeder Stations) katika maeneo ya Urafiki, Shekilango, Magomeni
Mapipa, Kinondoni, Mwinyijuma na Fire, hadi Aprili, 2014, maendeleo ya mradi
kwa jumla ni asilimia 45.
17. Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mbezi (Morogoro Road) – Malamba Mawili – Kinyerezi - Banana (km 14); mkataba wa mradi huu umesainiwa na maandalizi ya
ujenzi kwa kiwango cha lami yanaendelea.
Barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill – Goba - Mbezi Mwisho (km
20); mkataba
umesainiwa na maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami yanaendelea.
Barabara ya Tangi Bovu-Goba (km 9); nayo mkataba umesainiwa na maandalizi ya ujenzi kwa
kiwango cha lami yanaendelea.
Barabara ya Kimara Baruti-Msewe (km 2.6); Barabara hii inasaidia kupunguza msongamano wa magari
hasa katika barabara ya Morogoro kuingia na kutoka katikati ya jiji. Mkataba
umesainiwa na maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami yanaendelea.
18. Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kimara – Kilungule - External
Mandela Road (km 9); mkataba
wa awamu ya kwanza wa makutano ya barabara ya External na
Mandela hadi Maji Chumvi (km 3.0) umesainiwa na maandalizi ya kuanza ujenzi kwa
kiwango cha lami yanaendelea.
Barabara ya Kibamba – Kisopwa (km 12.0); Mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami umesainiwa. Aidha,
barabara ya Mwenge – Tegeta, Bagamoyo – Msata, Daraja la Kigamboni, Tazara
flyover na Barabara ya Rangi Tatu – Gerezani zipo kwenye hatua mbalimbali za
ujenzi. Wizara pia imenunua
kivuko kitakachofanya kazi kati ya Dar es Salaam – Bagamoyo ambacho kitawasili
nchini Juni, 2014. Pia hatua mbalimbali zinachukuliwa na Wizara yangu katika
kupunguza misongamano katika miji ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Iringa, Morogoro
na Mbeya.
19.
Mheshimiwa
Spika, miradi mingine
iliyotekelezwa katika mwaka 2013/14 ni vivuko, nyumba na majengo ya Serikali
ambayo utekelezaji wake umefafanuliwa katika Kitabu changu cha Hotuba ya Bajeti ukurasa 71 – 75 na utekelezaji wa miradi ya usalama barabarani
na mazingira, masuala mtambuka pamoja na Utekelezaji wa Bodi na Taasisi zilizo
chini ya Wizara umeonyeshwa katika ukurasa
75 -103.
20.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha
kuanzia Januari – Aprili, 2014 nchi yetu ilikumbwa na janga la mafuriko yaliyosababishwa na mvua
kubwa zilizonyesha katika mikoa yote.
Mafuriko hayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri zikiwemo
barabara na madaraja. Mikoa
14 iliyokumbwa na mafuriko hayo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro,
Mbeya, Ruvuma, Lindi, Mara, Tanga, Rukwa, Mtwara, Katavi, Dodoma, Iringa na
Arusha. Wizara kwa kupitia Wakala wa
Barabara ilifanya juhudi za kukarabati na kuimarisha maeneo yaliyokumbwa na
mafuriko hayo na hivi sasa yanapitika na wananchi wanapata huduma za usafiri
kama kawaida. Aidha, maeneo mengine yanaendelea kuboreshwa. Napenda kuwahakikishia
Wananchi kuwa barabara zote zitakarabatiwa ili zirudi katika hali yake ya
kawaida.
21.
Mheshimiwa
Spika, Aidha katika mwaka
wa fedha 2013/14 Wizara imeendelea na jitihada za kukabiliana na magari
yanayozidisha uzito barabarani. Athari
za uzidishaji wa mizigo ni pamoja na uharibifu wa barabara ambazo zimejengwa
kwa gharama kubwa. Tatizo hili limeathiri
kwa kiwango kikubwa barabara hapa nchini ikizingatiwa takribani asilimia 99.3
ya mizigo inayosafirishwa inatumia barabara.
Wizara imeendelea kuwaelimisha wasafirishaji pamoja na kufanya jitihada
za kudhibiti mianya ya rushwa kwenye mizani.
Mizani ya kisasa inayopima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh-In-Motion) inaendelea kujengwa katika
maeneo ya Vigwaza (Pwani), Mikese (Morogoro) na Nzuki (Singida). Aidha, Watumishi wenye elimu za Shahada na
Stashahada wameajiriwa kwenye mizani na kuboreshewa maslahi yao. Watumishi 461 walifukuzwa kazi kwenye mizani
kwa kukiuka maadili ya kazi kuanzia Agosti, 2012 hadi Aprili, 2014. Nawasihi
Watumiaji wa Barabara hasa Wasafirishaji wazingatie Sheria Na. 30 ya Mwaka 1973 ili barabara zetu zidumu.
C: MAKADIRIO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15
22.
Mheshimiwa
Spika, Wizara inatarajia kukusanya
Shilingi 41,123,000.00. Bajeti ya Matumizi
ya Kawaida ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2014/15, ni Shilingi 557,483,565,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi
24,338,319,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi, Shilingi 6,944,846,000.00 ni kwa ajili
ya Matumizi Mengineyo ya Wizara na Taasisi, na Shilingi 526,200,400,000.00 ni fedha za Mfuko wa Barabara.
23.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
ya Ujenzi imetengewa jumla ya Shilingi 662,234,027,000.00.
kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 450,000,000,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 212,234,027,000.00 ni fedha za nje. Mgawanyo wa fedha za maendeleo pamoja na miradi
iliyotengewa fedha ni kama inavyooneshwa katika Kiambatisho Na.1.
MIRADI YA VIVUKO NA NYUMBA ZA
SERIKALI
24.
Mheshimiwa
Spika, Ujenzi wa Maegesho ya Vivuko umetengewa Shilingi
Milioni 5,990.00 kwa ajili ya kazi za ujenzi wa maegesho ya kivuko cha Dar
es Salaam – Bagamoyo pamoja na upanuzi wa sehemu ya Maegesho ya Kigamboni,
Iramba – Majita, Bukondo na Zumacheli,
na maandalizi ya kuanzisha usafiri wa majini katika mwambao wa ziwa Victoria ili kupunguza
msongamano katika Jiji la Mwanza.
25.
Mheshimiwa
Spika, Ununuzi wa Vivuko Vipya umetengewa Shilingi
milioni 4,512.32 kwa ajili ya ununuzi
wa kivuko kitakachofanya kazi kati ya Magogoni – Kigamboni, ununuzi wa mashine
za kisasa za kukatia tiketi (ticket vending machines) kwa ajili ya vivuko vya
Kisorya, Ilagala na Pangani na ununuzi wa vifaa vya karakana za TEMESA katika
mikoa ya Manyara, Singida, Lindi, Mwanza, Kagera na Ruvuma.
26.
Mheshimiwa
Spika, Ukarabati Wa Vivuko umetengewa Shilingi
milioni 2,102.21 kwa ajili ya kukarabati vivuko vya MV Magogoni, MV Mwanza, ‘Tug boat’ MV Kiu- Morogoro na MV Pangani II- Tanga.
27.
Mheshimiwa
Spika, Ujenzi na Ukarabati wa Nyumba na Majengo ya Serikali umetengewa Shilingi milioni 2,689.46 kwa ajili ya kuendelea na
ujenzi wa nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo na ujenzi wa nyumba za
Majaji katika Mikoa ya Shinyanga (1),
Kagera (1), Mtwara (1), Kilimanjaro (1) na Dar es Salaam (1), na ujenzi wa
jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi (awamu ya nne). Aidha, kuendelea na ujenzi wa uzio na kuweka
mfumo wa ulinzi katika nyumba za viongozi wa Serikali zilizopo Mikocheni, Kijitonyama
na Msasani Peninsular, kufanyia matengenezo na ukarabati wa nyumba za viongozi
wa Serikali.
28.
Mheshimiwa
Spika, shughuli
nyingine ni ukarabati wa Karakana za TEMESA katika Mikoa ya Mwanza, Arusha, Dar
es Salaam, Dodoma na karakana za Vikosi vya Ujenzi.
MIRADI
YA BARABARA NA MADARAJA
29.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro (Km 200)
sehemu ya Dar es Salaam – Chalinze (Km 100) zimetengwa Shilingi
milioni 750.00. Shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuendelea na maandalizi
ya ujenzi kwa njia sita wa Awamu ya Kwanza ya mradi huo kiwango cha “Expressway” kwa ubia baina ya Serikali
na Sekta Binafsi (Public Private
Partnership – PPP). Aidha, Kiasi
cha Shilingi milioni 500.00 zimetengwa
kwa ajili ya kukarabati na kuimarisha (Backlog Maintenance) sehemu ya Mlandizi
– Chalinze (km 44.24).
30.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo – Msata zimetengwa Shilingi
Milioni 10,885.24. Shilingi
milioni 10,441.10 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara ya
Bagamoyo – Msata (km 64). Shilingi milioni 444.14 kwa ajili ya kukamilisha
usanifu wa kina kwa barabara ya Bagamoyo – Sadani – Tanga (km 178).
31.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Usagara – Geita – Kyamyorwa (km 422) sehemu
ya Uyovu – Biharamulo (km 112) zimetengwa shilingi milioni 9,800.00. Shilingi milioni 8,000.00 kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Uyovu –
Biharamulo (km 112), kiasi cha Shilingi
milioni 800.00 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Kyamyorwa
–Buzirayombo (km120) na kiasi cha Shilingi milioni 1,000.00 kwa ajili ya malipo
ya mwisho ya mkandarasi kwa sehemu ya Geita - Usagara (lot 1 na 2) (km 90).
32.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Kigoma – Kidahwe – Uvinza – Kaliua – Tabora
(Km 430) zimetengwa shilingi milioni 36,596.34 ambapo
Shilingi milioni 12,139.53 kwa ajili ya kuendelea na maungio ya barabara za
Daraja la Kikwete katika Mto Malagalasi na Shilingi milioni 3,581.95 kwa ajili
ya kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya mkandarasi wa barabara ya
Kidahwe-Uvinza (km 76.6).
33.
Mheshimiwa
Spika, Shilingi milioni
6,837.80 kwa ajili ya kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya mkandarasi wa
barabara ya Tabora - Ndono (km 42), Shilingi milioni 7,189.04 kuendelea na
ujenzi sehemu ya Ndono -Urambo (km 52) na kiasi cha Shilingi milioni 4,848.02
kwa ajili ya sehemu ya Kaliua – Kazilambwa (km 56). Kwa upande wa barabara ya
Uvinza – Malagarasi (km 51), Urambo – Kaliua (km 33) na Kazilambwa – Chagu (km
40) kiasi cha Shilingi milioni 2,000 zimetengwa.
34.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Marangu – Tarakea – Kamwanga/ Bomang’ombe –
Sanya Juu (km 173), Arusha Moshi – Holili (km 140), Same – Himo – Marangu na Mombo – Lushoto (km 132), KIA – Mererani (km 26), Kwa Sadala – Masama – Machame Jct (km
15.5) na Kiboroloni – Kiharara – Tsudini
– Kidia (km 10.80) zimetengwa
jumla shilingi milioni 13,133.63.
35.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Nangurukuru – Mbwemkulu (km 95) jumla
ya Shilingi milioni 2,000.00 zimetengwa.
36.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Dodoma – Manyoni (km 127) jumla
ya Shilingi milioni 1,309.28
zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara ya mchepuo kuingia
Manyoni mjini (km 4.8) na kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya Mkandarasi.
37.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Mbwemkuru – Mingoyo (km 95) imetengewa
kiasi cha Shilingi milioni 535.00.
38.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Nelson Mandela (km15.6) imetengewa Shilingi
milioni 1,500.00 kwa ajili ya kulipa malipo ya mwisho ya mkandarasi. Aidha,
kiasi cha Shilingi milioni 150.00
kimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya upanuzi wa barabara ya Nelson Mandela
sehemu ya Dar Port – TAZARA (km 6.0)
kuwa njia sita.
39.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Dumila – Kilosa (km 78) imetengewa Shilingi
milioni 8,000.00 kwa ajili ya kulipa madai ya Mkandarasi na kuendelea na
ujenzi wa sehemu ya Rudewa-Kilosa (km 24).
40.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Sumbawanga – Matai -Kasanga Port (km. 112) imetengewa
kiasi cha Shilingi milioni 10,241.37 kwa ajili ya kuendelea
na kazi za ujenzi.
41.
Mheshimiwa
Spika, Ujenzi
wa Madaraja ya Kirumi (Mara), Nangoo, Sibiti, Maligisu
(Mwanza), Kilombero, Kavuu, Mbutu, Ruhekei, Ruhuhu (Ruvuma), Momba, Simiyu, Wami, Lukuledi II na ununuzi wa Emergency Mabey Bridge Parts zimetengwa Shilingi
milioni
25,500.00.
42.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya New Bagamoyo (Kawawa Jct – Tegeta km 17.1) zimetengwa Shilingi Milioni
14,500.00
wakati barabara ya Kyaka – Bugene (km
59.1) jumla ya Shilingi milioni 6,037.53
zimetengwa.
43.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Isaka – Lusahunga (km 242), Lusahunga
– Rusumo na Nyakasanza – Kobero (km
150) zimetengwa Shilingi milioni 20,520.480. Aidha, barabara ya Manyoni - Itigi – Tabora (km 264) zimetengwa Shilingi milioni 21,499.57. Shilingi
milioni 10,000.00 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa sehemu ya Tabora – Nyahua
na Shilingi milioni 10,299.57 kwa sehemu
ya Manyoni – Itigi – Chaya. Kwa upande wa barabara ya Nyahua - Chaya (km 90) zimetengwa
Shilingi milioni 1,200.00 ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
44.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Korogwe – Handeni (km 65) Shilingi
milioni 6,356.73 zimetengwa na Barabara
ya Handeni – Mkata (km 54) zimetengwa Shilingi
Milioni 4,484.75 kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya mkandarasi.
45.
Mheshimiwa
Spika, barabara za Mikoa zimetengewa
Shilingi Milioni 31,915.27. Orodha ya miradi ya barabara za mikoa kwa
kutumia fedha za Bajeti ya Maendeleo imeonyeshwa katika Kiambatisho Na. 2 kwenye
kitabu changu cha Hotuba ya Bajeti.
46.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Mwandiga – Manyovu (km 60) imetengewa Shilingi
milioni 500.00 na Daraja la Umoja limetengewa Shilingi milioni 500.00 kwa ajili ya
kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya
mkandarasi.
47.
Mheshimiwa
Spika, barabara za Kuondoa Msongamano Dar es salaam (km 109.35) zimetengwa shilingi
milioni 28,945.00. Kiasi cha Shilingi milioni 605.00 kwa ajili ya
kukamilisha kazi zilizobakia kwa barabara ya Kawawa Roundabout - Msimbazi
Valley – Jangwani/Twiga Jct. Shilingi milioni 1,290.00 kwa ajili ya kulipa
sehemu ya madai ya mkandarasi wa barabara ya Jet Corner – Vituka - Devis
Corner, Shilingi milioni 2,500.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi barabara ya Ubungo
– Maziwa – External na Tabata Dampo – Kigogo, Shilingi milioni 5,000.00 kwa
ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Kimara – Kilungule – External, Shilingi
milioni 6,000.00 kwa ajili ya barabara ya Mbezi – Malambamawili – Kinyerezi –
Banana, Shilingi milioni 5,000.00 kwa ajili ya barabara ya Tegeta – Kibaoni –
Wazo Hill – Goba – Mbezi (Morogoro Road).
Shilingi milioni 3,000.00 ni kwa ajili ya barabara ya Tangi Bovu –
Goba, Shilingi milioni 1,500.00 kwa
ajili ya barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Changanyikeni, Shilingi milioni
1,500.00 kwa ajili ya barabara ya Kibamba – Kisopwa, Shilingi milioni 1,000.00
kwa ajili ya barabara Banana – Kitunda – Kivule – Msongola (km 14.7) na
Shilingi milioni 1,500.00 kwa ajili ya barabara ya Ardhi – Makongo. Aidha, kiasi cha Shilingi milioni 50.00 zitatumika
kufuatilia na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (Bus
Rapid Transit Infrastructure).
48.
Mheshimiwa
Spika, ujenzi wa flyovers Dar es Salaam na Barabara za
maingilio zimetengewa Shilingi milioni
19,150.00 ambapo Shilingi milioni 16,000.00 ni kwa ajili ya kuanza ujenzi
wa ‘Flyover’ ya TAZARA na Shilingi milioni 3,000.00 kwa ajili ya maboresho ya makutano ya
Chang'ombe, Ubungo, Uhasibu, KAMATA, Magomeni, Mwenge, Tabata/Mandela na
Morocco. Kiasi cha Shilingi milioni 150.00 zitatumika kwa ajili ya maandalizi
ya upanuzi wa barabara TAZARA – JNIA (km 6.0) kuwa njia sita.
49.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Ndundu - Somanga (km 60) imetengewa
Shilingi milioni 5,287.74 wakati barabara ya Kidatu –
Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha/Songea (km 396) imetengewa Shilingi milioni 1,600.00 kwa ajili ya
kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
50.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Tabora – Ipole – Koga – Mpanda (km 351.40) imetengewa Shilingi milioni 7,260.00. Shilingi milioni 2,560.00 ni kwa ajili
ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami
sehemu ya Mpanda – Koga – Ipole (km 261.40) na Shilingi milioni 4,700.00
kwa sehemu ya Tabora - Sikonge - Ipole
(km 90.00).
51.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Makutano – Natta – Mugumu/ Loliondo – Mto wa
Mbu (km 452) zimetengwa Shilingi milioni 9,617.63 ambapo jumla ya Shilingi milioni 5,617.63 ni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi
kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Makutano -Sanzate (km 50) na Shilingi
milioni 4,000.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha
lami sehemu ya Mto wa Mbu – Loliondo (km 213).
52.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Ibanda
– Itungi/Kiwira Port (km
26) zimetengwa Shilingi milioni 1,000.00
kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa barabara ya Ibanda – Itungi/Kiwira Port
sehemu ya Kajunjumele – Kiwira Port (km 5.6).
53.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Nzega – Tabora (km 115) zimetengwa Shilingi
milioni 13,169.34 ambapo Shilingi milioni 6,696.04 ni kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Nzega – Puge na Shilingi milioni 6,473.30 kwa
ajili ya sehemu ya Puge – Tabora.
54.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Sumbawanga – Mpanda – Uvinza (km 440.4) zimetengwa Shilingi milioni 28,858.72 ambapo Shilingi milioni 8,850.94 ni kwa
ajili ya kuendelea na kazi ya ujenzi wa sehemu ya Sumbawanga-Kanazi, Shilingi
milioni 8,850.94 kwa sehemu ya Kanazi-Kizi-Kibaoni na Shilingi milioni 6,617.63
kwa sehemu ya Kizi-Sitalike-Mpanda. Shilingi milioni 4,539.21 ni kwa ajili ya
kuanza ujenzi wa sehemu ya Mpanda-Mishamo (km 100).
55.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Nyanguge – Musoma (km 183) na Mchepuo wa Usagara – Kisesa (km 17) zimetengwa Shilingi milioni 19,235.26 ambapo Shilingi milioni 2,500.00 zitatumika kuendelea na kazi ya
ukarabati wa barabara ya Nyanguge – Simiyu/Mara Border (km 85.5), kiasi cha
Shilingi 7,235.26 kwa ajili ya ukarabati wa sehemu ya Simiyu /Mara Border –
Musoma (km 80). Kiasi cha Shilingi milioni 4,000.00 kwa sehemu ya barabara ya
Kisesa – Usagara Bypass. Aidha, kiasi cha Shilingi milioni 4,500.00 kwa ajili
ya ujenzi wa barabara ya Nansio - Kisorya – Bunda - Nyamuswa sehemu ya Kisorya
- Bunda (km 50) na Shilingi milioni 1,000.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi
sehemu ya Nyamuswa - Bunda.
56.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Magole – Mziha (Magole – Turiani km 48.8) jumla ya Shilingi
milioni 6,156.84 zimetengwa
kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
57.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi (km
171.8) (Bariadi – Lamadi km 71.8) zimetengwa Shilingi Milioni 10,965.65.
Shilingi milioni 6,465.65 kwa ajili ya barabara ya Bariadi – Lamadi (km
71.8) na kiasi cha Shilingi milioni
4,500.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
barabara ya Mwigumbi - Maswa - Bariadi (km 100). Zabuni zimetangazwa kwa
sehemu ya Mwigumbi – Maswa.
58.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Tabora – Ipole – Rungwa (Ipole – Rungwa km
95) imetengewa Shilingi milioni 50.00. kwa ajili ya
kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
59.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo - Nyakanazi (km 310) jumla ya
Shilingi milioni 10,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na
ujenzi wa kilomita 100 za barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi (km
310) kwa kiwango cha lami. Mikataba ya ujenzi kwa sehemu ya Kidahwe – Kasulu
(km 50) na Nyakanazi – Kibondo (km 50) imekwishasainiwa na makandarasi wako
kwenye maeneo ya kazi (sites) kwa ajili ya ujenzi.
60.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya kuingia uwanja wa ndege wa Mafia (Mafia Airport
Access Road km 14) jumla ya Shilingi
milioni 2,471.17 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango
cha lami.
61.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Chuo Kikuu cha Dodoma (km 12) jumla ya Shilingi
milioni 3,000.00 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango
cha lami.
62.
Mheshimiwa
Spika, daraja la Kigamboni na barabara za maingilio ya kwenye
daraja zimetengwa Shilingi milioni 7,451.56 ambapo Shilingi milioni 4,951.56 ni kwa ajili
ya kuendelea na kazi ya ujenzi wa daraja, na Shilingi milioni 2,500.00 kwa
ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya maingilio ya Mjimwema – Vijibweni (km 10).
63.
Mheshimiwa
Spika, ujenzi wa njia za magari mazito na maegesho ya dharura
kwa ajili ya kuimarisha barabara katika ukanda wa kati Shilingi milioni 200.00 zimetengwa.
64.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya PUGU sehemu ya JNIA – Pugu (km 8.0) jumla ya Shilingi
milioni 150.00 zimetengwa kwa ajili ya kuanza usanifu ili kuipanua kuwa
njia sita.
65.
Mheshimiwa
Spika, kuipanua barabara ya Kimara – Kibaha ikijumuisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji jumla ya Shilingi milioni 250.00 zimetengwa kwa ajili ya kuanza usanifu.
66.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Kisarawe – Mlandizi (km 52) jumla ya Shilingi
milioni 400.00 zimetengwa kwa ajili ya kuanza usanifu wa kujenga kwa kwa
kiwango cha lami. Aidha, upanuzi wa barabara
ya Bandari (km 1.2), ujenzi wa barabara
ya Dockyard (km 0.7) na Mivinjeni
(km 1.0) jumla ya Shilingi milioni 50.00
zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi.
67.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Pugu – Kifuru – Mbezi Mwisho – Mpiji Magoe –
Bunju (km 34) kuwa njia
tatu Shilingi milioni 1000.00 zimetengwa
ambapo jumla ya Shilingi milioni 500.00 ni kwa ajili ya kuanza usanifu wa
sehemu ya Pugu – Kifuru – Mbezi Mwisho (km 12.7) na Shilingi milioni 500.00 ni
kwa ajili ya kuanza usanifu wa sehemu ya Mbezi Mwisho – Magoe Mpiji – Bunju (km
21.3).
68.
Mheshimiwa
Spika, kujenga mizani mipya karibu na bandari ya Dar es Salaam Shilingi milioni 100.00 zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya
usanifu. Aidha, barabara ya Tunduma –
Sumbawanga (km 224.81) Shilingi
milioni 1,057.88 zimetengwa ambapo Shilingi milioni 57.88 ni kwa ajili ya
kuhamisha miundombinu katika eneo la Tunduma – Sumbawanga na kiasi cha Shilingi
milioni 1,000.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa sehemu ya Tunduma mjini (km
1.6).
69.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Kagoma – Lusahunga (km 154) Shilingi
milioni 9,600.00 zimetengwa kulipa sehemu ya madai ya mkandarasi wakati barabara ya Arusha – Namanga (km 105) imetengewa
Shilingi milioni 4,517.12.
70.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Singida – Babati – Minjingu –
Arusha (km 321.5) imetengewa shilingi
milioni 10,444.83 kwa ajili ya kuendelea na
ukarabati wa barabara ya Minjingu hadi Arusha yenye urefu wa kilomita 98
na barabara ya Dar es salaam – Mbagala
(Kilwa Road) – Gerezani (sehemu ya
Kamata – Bendera Tatu km 1.5) imetengewa Shilingi milioni 8,000.00 kwa ajili ya kukamilisha ulipaji fidia na kuanza ujenzi wa
sehemu ya KAMATA – Bendera Tatu (km 1.5).
71.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Msimba – Ruaha/Ikokoto Mafinga (km 517.40) zimetengwa
Shilingi milioni 43,284.28 ambapo Shilingi milioni 4,016.513 ni kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya
mkandarasi barabara ya Iringa – Mafinga (Km 68.9); Shilingi milioni 34,844.527 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya
Mafinga-Igawa yenye urefu wa kilometa 137.9. Aidha, Shilingi milioni 500 kwa
ajili ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa
barabara ya Igawa-Madibira-Mafinga, Shilingi milioni 2,823.24 kwa ajili
ya ujenzi wa Njombe-Ndulamo-Makete,
na Shilingi milioni 1,000.00
kwa ajili ya ujenzi wa Njombe-Lupembe-Madeke.
72.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Korogwe - Mkumbara –Same (km 172) imetengewa shilingi
milioni 15,200.00.
73.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Mbeya - Makongolosi (km 115) shilingi
milioni 13,340.12 ambapo Shilingi milioni 6,528.78 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa sehemu ya
Mbeya-Lwanjilo; Shilingi milioni 5,008.00 kwa sehemu ya Lwanjilo-Chunya na
Shilingi milioni 1,495.50 kwa sehemu ya Chunya – Makongolosi. Aidha, Shilingi
milioni 307.84 kumalizia deni la
Mhandisi Mshauri aliyefanya kazi ya usanifu wa kina wa sehemu ya Makongolosi –
Rungwa – Itigi – Mkiwa.
74.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Chalinze – Segera – Tanga (km 248) zimetengwa
shilingi milioni 3,500.00 ambapo Shilingi
milioni 2,500.00 kwa ajili ya kulipa
sehemu ya madai ya mkandarasi wa sehemu ya Kitumbi-Segera-Tanga. Aidha,
Shilingi milioni 1,000.00 ni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara ya
Msoga – Msolwa (Chalinze Bypass).
75.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Itoni – Ludewa – Manda (km
211) jumla ya Shilingi milioni 4,400.00
zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa sehemu ya kilometa 50 za barabara ya
Itoni – Ludewa – Manda.
76.
Mheshimiwa
Spika, Daraja la Ruvu Chini kwenye barabara ya Bagamoyo – Msata Shilingi milioni 700.00 zimetengwa.
77.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Dodoma – Mtera – Iringa (km 260) imetengewa Shilingi
milioni 21,739.31 na barabara ya Dodoma
– Kondoa – Babati (km 261) zimetengwa Shilingi
milioni 28,392.41.
78.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya Masasi- Songea – Mbamba Bay (km 659.7) zimetengwa Shilingi milioni 68,383.08 ambapo Shilingi milioni 10,533.88 kwa
ajili ya kuendelea na ujenzi Mangaka-Nakapanya; Shilingi milioni 10,532.57 kwa Nakapanya
– Tunduru; Shilingi milioni 10,532.93 kwa
sehemu ya Mangaka-Mtambaswala; na Shilingi milioni 10,567.32 kwa Tunduru-Matemanga;
Shilingi milioni 10,679.20 kwa Matemanga-Kilimasera; Shilingi milioni 10,679.18
kwa Kilimasera – Namtumbo. Aidha, fedha kwa ajili ya gharama za usimamizi na
ufuatiliaji wa mradi katika kipindi cha uangalizi ni Shilingi milioni 17.00 kwa
barabara ya Songea – Namtumbo na Shilingi milioni 17.00 kwa barabara ya Peramiho – Mbinga. Shilingi milioni 2,324.00 ni
kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Mbinga-Mbamba Bay, na
Shilingi milioni 2,500.00 kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Masasi - Newala – Mtwara.
79.
Mheshimiwa
Spika, Ujenzi Makao Makuu ya Wakala wa Barabara pamoja ujenzi wa Ofisi za mikoa ya Dar es Salaam,
Katavi, Geita, Simiyu, Njombe na Lindi, jumla ya Shilingi milioni 2,934.35 zimetengwa kwa ajili ya kuanza kazi ya
ujenzi.
80.
Mheshimiwa
Spika, barabara ya kuingia
kwenye Chuo cha Uongozi pamoja na barabara
zilizoko ndani ya Chuo hicho jumla ya Shilingi
milioni 1,500.00 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi.
81.
Mheshimiwa
Spika, mradi
wa Usalama Barabarani zimetengwa Shilingi
milioni 4,899.00; Usalama, Mazingira na Marekebisho ya Mfumo
- Shilingi milioni 720.00; Menejimenti na Utunzaji wa Mazingira – Shilingi milioni 502.34 ambapo
mchanganuo wa miradi yote hii na kazi zitakazofanyika zimeainishwa katika
Kitabu cha Hotuba yangu Ukurasa 155 - 158.
82.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka wa fedha 2014/15, Mfuko wa
Barabara unatarajiwa kukusanya jumla ya Shilingi 751,700,000,000.00. Mchanganuo wa fedha za Mfuko wa Barabara zilizotengwa
kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi umeonyeshwa katika Kiambatanisho Na. 3.
83.
Mheshimiwa
Spika, maelezo ya miradi
ya barabara na shughuli zingine zinazotekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa
Barabara kwa mwaka wa fedha 2014/15 yameainishwa kwenye Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ukurasa 159 - 175. Aidha, fedha za matengenezo ya barabara kuu na barabara za
mikoa kwa mwaka wa fedha 2014/15 kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ni
jumla ya Shilingi 469,494,900,00.00.
Mchanganuo wa mpango huo wa matengenezo umefafanuliwa
katika ukurasa 175 - 179 na katika
Viambatisho
Na. 5A hadi 5E katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
MPANGO WA UTEKELEZAJI KAZI KATIKA TAASISI ZILIZO CHINI YA
WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15
84.
Mheshimiwa Spika, shughuli zitakazofanywa na Wakala
wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Bodi ya Mfuko wa Barabara zimefafanuliwa
katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti Ukurasa
179 - 183.
85.
Mheshimiwa
Spika, Bodi ya Usajili
wa Wahandisi imepanga kusajili
Wahandisi 800, Mafundi Sanifu 200 na Kampuni za Ushauri wa Kihandisi 25. Bodi
pia itasimamia mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wahitimu 692 ambapo
wahandisi wahitimu 442 ni wanaoendelea na 250 watakuwa wapya. Vile vile bodi
itaendelea kuwaapisha wahandisi wataalamu na wahandisi washauri wote
waliosajiliwa na wanaoendelea kusajiliwa ili kuhakikisha kuwa wahandisi
wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria. Hivyo Waheshimiwa
Wabunge wenye fani ya uhandisi mnaombwa mjitokeze kwa ajili ya viapo hivyo
muhimu katika fani ya uhandisi.
86.
Mheshimiwa
Spika, Bodi ya Usajili
wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi inatarajia kusajili Wabunifu Majengo 25, Wakadiriaji Majenzi 35, Kampuni 24 za Wabunifu Majengo na 10 za
Wakadiriaji Majenzi. Aidha, Bodi itaendelea kukagua shughuli za wataalamu hao
kwenye miradi iliyopo nchini inayostahili kukaguliwa kwa mujibu wa sheria.
87.
Mheshimiwa
Spika, Bodi ya Usajili
wa Makandarasi imepanga kusajili jumla ya Makandarasi 834 wa fani
mbalimbali pamoja na kukagua miradi ya
ujenzi 2,500. Aidha, Bodi itaendesha
kozi tano za mafunzo kwa makandarasi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga,
Mara, Rukwa na Dodoma. Bodi pia itaendeleza Mfuko Maalum wa Kutoa Dhamana ya
Kusaidia Makandarasi Wadogo na wa Kati (Contractors Assistance Fund), jitihada
za kuhamasisha makandarasi wazalendo kujiunga ili kuomba zabuni kwa mfumo wa
ubia na mkutano wa mafunzo ya utekelezaji wa miradi kwa ubia kwa makandarasi wa
Kanda ya Kusini utafanyika mjini Iringa.
88.
Mheshimiwa
Spika, shughuli za
Taasisi nyingine chini ya Wizara yangu kama vile Baraza la Taifa la Ujenzi,
Vikosi vya Ujenzi, Chuo cha Ujenzi
Morogoro, Chuo cha Matumizi
ya Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi (Appropriate Technology Training Institute –
ATTI) cha Mbeya, Kituo cha Usambazaji
wa Teknolojia Katika Sekta ya Uchukuzi (Tanzania Transportation Technology
Transfer Centre) na Masuala Mtambuka ya Maendeleo ya Rasilimali Watu, Habari,
Elimu na Mawasiliano, Ushirikishwaji wa Wanawake Katika Kazi za Barabara
Nchini, Mikakati ya Kupambana na UKIMWI, Kudhibiti Rushwa na Mapitio ya
Sera ya Ujenzi zimeainishwa katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ukurasa 186 -
192
SHUKURANI
89.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, napenda
kuwashukuru kwa dhati wale wote walioshirikiana nasi katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2013/14 katika kutimiza malengo yetu. Shukrani za pekee ziwaendee
Washirika wa Maendeleo walioendelea kushirikiana nasi katika kutekeleza
programu na mipango yetu katika kuendeleza Sekta ya Ujenzi. Washirika hao ni
pamoja na Abu Dhabi, Denmark (DANIDA), Japan (JICA), Korea, Marekani (MCC), Uingereza
(DFID), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Benki ya Dunia (WB), Benki ya
Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA), Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya
Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Kuwait Fund, SIDA
na OPEC Fund.
90.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru
viongozi wenzangu katika Wizara nikianzia na Mhe. Eng. Gerson H. Lwenge (Mb.), Naibu Waziri; Eng.
Mussa I. Iyombe, Katibu Mkuu na Eng.
Joseph M. Nyamhanga, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi. Aidha, ninawashukuru Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi
zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Vitengo pamoja na wafanyakazi
wote wa Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake, kwa kujituma na kujitolea kwa juhudi
na maarifa katika kutekeleza malengo na
majukumu ya Wizara yetu.
91.
Mheshimiwa
Spika, tunawashukuru
wadau wote wa sekta ya ujenzi, na hasa sekta binafsi, ambao wametupa
ushirikiano wa kutosha katika kuendeleza sekta hii. Aidha, nachukua fursa hii kuvipongeza vyombo mbalimbali
vya habari kwa ushirikiano wao na jinsi ambavyo vimekuwa vikifuatilia na kutoa
taarifa za shughuli zinazohusiana na malengo, sera, sheria na kanuni mbalimbali
zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi. Shukrani zangu za dhati pia nazitoa kwa
Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa
Serikali kwa kuchapa hotuba hii.
92.
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee nawashukuru wapiga kura
wangu wa Jimbo la Uchaguzi la Chato kwa ushirikiano wanaonipatia na uvumilivu
wao kipindi chote ninapotekeleza majukumu ya Kitaifa.
93.
Mheshimiwa
Spika, hotuba yangu hii
inapatikana katika tovuti ya Wizara ya Ujenzi - (www.mow.go.tz).
MAOMBI YA FEDHA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2014/15
94.
Mheshimiwa
Spika, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake ya
kuendeleza sekta ya ujenzi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
liidhinishe jumla ya Shilingi 1,219,717,592,000.00
kwa
ajili ya matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2014/15. Kati ya
fedha hizo, Shilingi 557,483,565,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambazo zinajumuisha
Shilingi 24,338,319,000.00 za mishahara ya Watumishi (PE), Shilingi 6,944,846,000.00 za matumizi mengineyo (OC) na Shilingi 526,200,400,000.00 za Mfuko wa Barabara.
Bajeti ya
Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 662,234,027,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi
450,000,000,000.00 ni
fedha za ndani na Shilingi 212,234,027,000.00 ni
fedha za nje.
95.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment