WAOMBA HIFADHI NZURI YA MAKABURI YA MV BUKOBA


Serikali imeshauriwa kuweka mandhari nzuri ya makaburi ya pamoja ya marehemu wa ajali ya meli ya Mv Bukoba yaliyopo Igoma jijini Mwanza, na kushiriki katika kumbukumbu kwani watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi hufika katika eneo hilo la kumbukumbu. 
Hayo yalielezwa jana na baadhi ya ndugu wa marehemu waliozikwa katika eneo hilo, katika kumbukumbu ya miaka 18  tangu meli hiyo ilipopinduka na kuzama ndani ya Ziwa Victoria. 
“Suala la usafi katika eneo hili halitiliwi maanani kabisa na kumekuwa na wageni wanaotoka nje na ndani ya nchi wanaopaswa kukuta mandhari kama hii ikiwa safi ikizingatia kuwa eneo hilo ni la kihistoria kwa ajali iliyotokea,” alisema Hilda Justus. Akiongoza misa kwenye eneo la makaburi  Igoma, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Mimii Mziray, alitaka Serikali ijifunze kwa yale yaliyotokea miaka 18 iliyopita. 
“Mungu ametupatia wataalamu ili wafanye kazi mbalimbali zikiwemo za ufundi, lakini tumekuwa tukisafirisha watu kwa vyombo vibovu huku tukiwa na imani kuwa kwa mapenzi ya Mungu watafika salama,”  alisema na kuongeza kuwa maelezo yaliyotolewa baada ya ajali yalieleza kuwa meli ile ilikuwa na shida. 
Mwanamitindo wa kimataifa, Flaviana Matata ni miongoni mwa waathirika wa ajali hiyo ambapo alimpoteza mama yake mzazi, Beatrice Matata. 
Akizungumza katika kumbukumbu hiyo, Balozi Mwanaidi Majar  Sinare, alisema marehemu waliozikwa katika makaburi hayo wamekufa katika mazingira ambayo hayawezi kusahaulika. 
“Kumbukumbu hii inatoa nafasi ya kukumbuka nyuma tulipotoka  na kama kuna sehemu uzembe ulifanyika basi parekebishwe, ili ajali ya namna hiyo istokee tena,” alisema 

No comments: