WAGONJWA WAPYA 21 WA DENGUE WAGUNDULIKA

Ugonjwa wa homa ya dengue umeendelea kuwasumbua wakazi wa Dar es Salaam, ambapo wagonjwa wengine 21 waligundulika kupatwa na ugonjwa huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba, ilisema Hospitali ya Temeke ina wagonjwa 13, Kinondoni watatu na Ilala wanne.
“Kati ya wagonjwa hao 21 ni mmoja tu aliyepata matibabu na kuruhusiwa lakini wengine 20 wameendelea kulazwa kutokana na hali zao,” alisema Mkamba.
Aidha, alisema mapambano dhidi ya ugonjwa wa dengue, si ya Serikali peke yake, bali wananchi wote na kutaka ushirikiano zaidi kutokomeza mazalia ya mbu na kuweka mazingira katika hali ya usafi kuzuia mbu kuzaliana.
Alisema mbali na Serikali kupuliza dawa katika kata 78 jijini humo, kuliko na idadi kubwa ya waathirika wa ugonjwa huo, mabasi yaendayo mikoani yanaendelea kupuliziwa dawa ya kuua mbu, kuhakikisha mbu hawasafiri kuenea zaidi nchini.
Taarifa ya juzi inaonesha kuwa Hospitali ya Temeke ilipokea wagonjwa wanane, Ilala wagonjwa 11, Kinondoni wagonjwa 17, Sinza mgonjwa mmoja na Kinondoni kwa Dk Mvungi mgonjwa mmoja.
Mpaka sasa watu 926 wameugua ugonjwa huo tangu ulipoanza mwaka huu.

No comments: