JAJI AJITOA KESI YA GHOROFA LILILOPOROMOKA DAR

Jaji Sheikh Razia amejitoa kusikiliza ombi la marejeo ya amri na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kubadilisha mashitaka na kufuta dhamana kwa washitakiwa tisa.
Washitakiwa hao ni wa kesi ya mauaji ya watu 27, yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam na huyo ni Jaji wa pili kujitoa, baada ya Jaji John Utamwa.Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kusikilizwa. Hata hivyo, Jaji Razia alijitoa kwa madai ana maslahi katika ombi hilo.
Alisema awali alikuwa radhi kusikiliza shauri hilo, lakini aligundua ana maslahi.Katika ombi lao, washitakiwa wanaiomba Mahakama Kuu kutathmini na kufanya marejeo ya mwenendo na amri, iliyotolewa Machi 12 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujiridhisha usahihi na uhalali wa mwenendo na amri hiyo.
Aidha, wanaiomba Mahakama kufuta hati ya mashitaka ya mauaji, ambayo wanadai ipo kinyume cha sheria na kuirejesha ya mauaji ya kutokukusudia, waliyokuwa wanakabiliwa nayo awali na iwape dhamana.
Washitakiwa waliowasilisha ombi hilo ni Raza Ladha, Godluck Mbaga, Wilbroad Mugabisyo, Ibrahim Kisoki, Charles Ogare, Zonazea Oushoudada,  Michael Hemed, Albert  Mnuo na Joseph  Ringo.
Awali, washitakiwa hao walikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya kutokukusudia, wakapewa dhamana, Machi 12 mwaka huu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliondoa hati hiyo na kuwafungulia kesi ya mauaji isiyo na dhamana.
Ombi hilo limeahirishwa hadi Juni 2 mwaka huu kupangiwa jaji.

No comments: