KESI YA ZITTO KABWE KUSIKILIZWA JULAI 31

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Julai 31 mwaka huu kusikiliza mapingamizi ya pande zote katika kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto dhidi ya chama hicho.
Jaji John Utamwa alisema hayo jana baada ya kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa mawakili wa Zitto hawakuwepo mahakamani.
Katika kesi hiyo, Zitto anaomba Mahakama itoe zuio kwa Kamati Kuu au chombo chochote cha chama, kujadili uanachama wake hadi atakapokata rufaa ya kupinga uamuzi uliomvua uongozi wa chama.
Anaomba Mahakama imwamuru Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa ampe nakala zinazotoa sababu za uamuzi wa kumvua uongozi katika kikao kilichofanyika Novemba 22 mwaka jana, ili akate rufaa katika Baraza Kuu la Chama.
Aidha, anaomba Mahakama iamuru Chadema isiingilie kazi zake za ubunge wala uanachama wake.Zitto amefungua kesi hiyo dhidi ya Baraza la Wadhamini la chama hicho na Dk Slaa.
Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa, Mahakama ilitoa amri kwa Kamati Kuu au chombo chochote cha Chadema, kutojadili uanachama wa Zitto hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Zitto alivuliwa wadhifa wake Chadema, sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa kilichodaiwa ni usaliti kwa chama hicho.

No comments: