KITUO CHA DALADALA MWENGE KUFUNGWA RASMI JUMAPILI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kufunga kituo cha daladala cha Mwenge, Jumapili, Juni Mosi mwaka huu.
Imewataka wamiliki, madereva na abiria wote kuanzia Jumatatu asubuhi Juni 02 mwaka huu, kutumia Kituo cha Makumbusho tu.
Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa na Sumatra jana na kusainiwa na Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo Kanda ya Mashariki, Conrad Shio.
Shio alisema kuwa sababu ya kufunga kituo hicho ni ufinyu wa eneo hilo.
Alisema ufinyu huo, unachangia dadalada kushindwa kuingia kituoni kwa wakati, hasa kipindi vya asubuhi na jioni, hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika eneo la Mwenge.
“Madereva mnatakiwa kutii agizo hili ili kuepuka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya yeyote atakayekaidi, aidha abiria mnaagizwa kutolazimisha kushushwa eneo hilo,” alieleza.
Shio alisema barabara za kuingia na kutoka kituo cha Makumbusho , zinaendelea kukarabatiwa na Manispaa ya Kinondoni, kuondoa tatizo la kuingia kituoni hapo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, eneo hilo la Mwenge kwa sasa litabaki kuwa eneo la wazi.

No comments: