MWILI WA MWIMBAJI AMINA NGALUMA KUWASILI DAR KESHO, KUZIKWA JUMAMOSI

Wanamuziki na wadau mbalimbali wa muziki wa dansi nchini wanakutana leo asubuhi hii kwenye Ukumbi wa Vijana Social Hall, uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kusaidia na kushiriki mazishi ya mwimbaji mahiri wa kike, Amina Ngaluma 'Japanese' aliyefariki Alhamisi iliyopita nchini Thailand.
Kwa mujibu wa mratibu wa kikao hicho, Mwinjuma Muumini, kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi huo uliopo jirani kabisa na Ukumbi wa Mango Garden kuanzia Saa 5:00 asubuhi ambapo mume wa marehemu, Rashid Sumuni anatarajiwa kuwa miongoni mwa watakaohudhuria.
Muumini alisema, lengo la kuitisha kikao hicho ni kuweza kuona wadau wa muziki na wanamuziki watakavyoweza kushirikiana na familia ya marehemu kuanzi hatua ya kupokea mwili wa Amina hadi mazishi kutokana na ukweli kwamba familia hiyo imetumia ghama kubwa kwa msiba huo kwa wiki nzima sasa.
Mwili wa Amina Ngaluma unatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kesho Ijumaa Saa 3:30 usiku kwa ndege ya Shirika la KLM na mazishi yake yatafanyika Jumamosi mchana.
Taarifa zote muhimu zitatolewa katika kikao hicho kinachoshirikisha pia Shirikisho la Muziki Tanzania na Muumini ametoa wito kwa wanamuziki wote na wadau kujitokeza kwa wingi katika kikao hicho ambacho kinatarajiwa kufungua njia mpya ya ushirikiano miongoni mwa wanamuziki nchini hasa wakati wa matatizo.
Marehemu Amina Ngaluma alikuwa nchini Thailand kwa shughuli za kimuziki hadi mauti yalipomfika Alhamisi iliyopita.
Marehemu ambaye aliwahi kutamba sana na bendi ya Tamtam akiwa na Mwinjuma Muumini, alikuwa shabiki mkubwa wa klabu ya soka ya Simba 'Wekundu wa Msimbazi'.

No comments: