WABUNGE WAOMBA KUPATIWA OFISI WAKIWA DODOMA



Wabunge wameendelea kupigia debe maslahi mazuri sanjari na mazingira bora ya kufanyia kazi kwa kutaka pamoja na masuala mengine, serikali iangalie uwezekano wa kumpatia kila mbunge ofisi ya kufanyia kazi awapo Dodoma.
Ushauri huo umetolewa  jana mjini hapa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Mjumbe wa kamati hiyo, Fakharia Shomar katika taarifa ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alisema kamati inapongeza Ofisi ya Spika pamoja na Tume ya Utumishi wa Bunge kwa kuendelea kutoa ushauri na mapendekezo kwa Rais ya kuboresha maslahi ya wabunge na watumishi wa bunge.
Alisema ili kuhakikisha bunge linatekeleza majukumu yake ipasavyo, wabunge wote wapatiwe ofisi za kufanyia kazi wanapokuwepo Dodoma ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa umakini na ufanisi.
Wakati ofisi ya Bunge imeingia mkataba na kampuni ya bima ya Jubilee kutoa matibabu kwa wabunge na familia zao, kamati imeshauri kampuni hiyo ielekezwe itoe elimu kwao kuhusu utaratibu wa utoaji huduma, aina ya matibabu na hospitali zinazohusika na mkataba huo na zinakopatikana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kamati, ofisi ya Bunge imeingia mkataba na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kujenga ofisi 178 za wabunge katika majimbo ambayo hayana ofisi.
Wabunge kupitia kamati hiyo, pia wameshauri ofisi ya bunge ihakikishe inaingia mikataba na benki zinazotoa mikopo yenye bima kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na deni la mkopo huo kwa familia za wabunge endapo watapoteza maisha kwa namna moja au nyingine.
Kamati imekuja na ushauri huo wakati kwenye bajeti ya 2014/15 ikiwa, kati ya Sh 224,932,198,000 zilizotengwa kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, zaidi ya nusu ni za mfuko wa bunge.
Taasisi nyingine ni Ofisi ya  Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotengewa Sh 20,732,781,000 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Sh 4,371,895,000.
Mfuko wa Bunge umeomba jumla ya Sh 123,941,455,000 ambazo kati yake, Sh 15,520,327,000 zinaombwa kwa ajili ya mishahara ya wabunge na watumishi, Sh 108,421,128,000 zitatumika kuendesha mikutano ya Bunge na Kamati pamoja na shughuli zingine za kiutawala.

No comments: