ABIRIA WA BODABODA KATIKATI YA JIJI KUKAMATWAMeya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi amesema abiria watakaokutwa wakiwa wamepanda pikipiki (bodaboda) katika maeneo ambayo pikipiki hizo hazina leseni ya kufanya biashara, watakamatwa na kufikishwa mahakamani pamoja na dereva.
Alisema pia wafanyabiashara ndogo, watakaokutwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, ikiwemo maeneo ambayo yamefanyiwa usafi na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni, watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Alisema hayo mjini Tanga jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambao walitaka kufahamu msimamo wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kuhusu kunyanyaswa kwa waendesha bodaboda katika maeneo mbalimbali nchini.
Dk Massaburi mbaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa ALAT, alisema Jumuiya hiyo imekuwa bega kwa bega na kuwaunga mkono waendesha bodaboda nchini, pale wanapofanya biashara zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Alisema zaidi ya kuwaunga mkono serikali za mitaa, zimekuwa pia zikiwawezesha vijana  kwa kuwapa mikopo na kuwapa nyenzo mbalimbali, zikiwemo bodaboda zenyewe  ili kukabiliana na maisha, hatua inayoonesha kuwa si kweli kwamba serikali haiwapi umuhimu waendesha bodaboda.
Akizungumzia agizo la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam la kuwazuia waendesha bodaboda na wafanyabiashara ndogo, kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, ikiwemo kuingia katikati ya Jiji, Dk Massaburi alisisitiza kuwa agizo hilo liko pale pale, kwa vile lipo kisheria.
Alisema ili kuonesha kuwa Halmashauri ya Jiji inatilia mkazo agizo hilo, kuanzia sasa abiria atakayekutwa akiwa amepanda pikipiki katika eneo ambalo haina leseni ya kufanya biashara hiyo, atakamatwa sambamba na dereva na kufikishwa mahakamani mara moja.
Alisema hatua kama hizo pia zitachukuliwa kwa wafanyabiashara watakaokutwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria yakiwemo yale  yaliyovunjwa na Jiji hivi karibuni katika operesheni ya kusafisha Jiji la Dar es Salaam.
Alisema kampeni hiyo haina maana kwamba Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haina mpango wa kuwaendeleza wafanyabiashara ndogo kama inavyopotoshwa, kwani ipo mipango kabambe ya kuboresha biashara ndogo katika Jiji hilo kwa kujenga maeneo maalumu  na ya kisasa ya kufanyia biashara hizo.
“Upo mpango wa uboreshaji wa maeneo ya biashara katika Jiji la Dar es Salaam unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo karibu dola milioni 100 zimetengwa kwa mradi huu.
“Huu ni uthibitisho wa Jiji kuelewa umuhimu wa kuwa na maeneo maalumu ya kufanyia biashara, na si kuruhusu biashara holela zinazoashiria ukiukwaji mkubwa  wa sheria. Tutasimama kidete kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge,” alisema Dk Massaburi.
Kauli hiyo ya Dk Massaburi imekuja wakati Umoja wa Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam chini ya Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kusema kuwa unajiandaa kutoa shinikizo la kuzuia kuendelea kwa kampeni hiyo ya usafi jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa inawaonea na kuwakandamiza wananchi wa kipato cha chini wakiwemo waendesha bodaboda.
Wabunge hao wamekuwa wakimrushia lawama za moja kwa moja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na Meya Massaburi kuwa  ndio vinara wa unyanyasaji huo, lakini viongozi hao wamekuwa wakipuuza madai hayo kwa maelezo kuwa  wanasimamia sheria zilizotungwa na wabunge wenyewe.

No comments: