TPA YAWEKEZA MABILIONI KUIMARISHA MIUNDOMBINUMamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema imewekeza zaidi ya dola milioni 500 na kupata mikopo yenye riba nafuu kutoka Benki ya Dunia na nchi mbalimbali za Ulaya katika kuendeleza miundombinu na manunuzi ya vifaa mbalimbali.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA,  Janeth  Ruzangi alisema hayo Dar es Salaam na kuyataja maeneo ya uendelezwaji kuwa ni pamoja na magati na maeneo ya kuhifadhi mizigo, vifaa vya kupakia na kupakua, vifaa vya majini na majengo.
Alisema chini ya uendelezaji miundombinu pia bandari imeongeza vifaa vya kuhudumia mizigo, sambamba na mabadiliko ya mfumo mzima wa mabadiliko ya ubebaji mizigo, usalama wa Bandari, pamoja na vifaa vya doria kuimarishwa.
Vilevile alisema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameongezeka katika shughuli za bandari na hivyo kuongeza tija na ufanisi.
Alisema Bandari ya Dar es Salaam  ni kubwa kuliko zote ikiwa na urefu wa kilomita 2.6 na upana wa mita 500 na ina uwezo wa kuhudumia tani milioni 10.1.
“Bandari ina magati 11, gati Na. 1 - 7 linahudumia shehena mchanganyiko na linaendeshwa na Mamlaka na Gati Na. 8 - 11 yanahudumia shehena ya kontena na yana uwezo wa kuhudumia kontena 330,000 kwa mwaka,” alisema.
Alivitaja vitengo vingine ni pamoja na kituo cha kuhudumia mafuta,  kituo cha nafaka  na karakana ndogo ya kukarabati meli, Mashedi 10 ya mizigo, Kitengo cha kuhudumia meli za mwambao na  Kitengo cha Nafaka chenye uwezo wa kuhifadhi tani 30,000.
Alisema kabla ya Uhuru, lango lilikuwa na uwezo wa kuingiza meli zenye urefu wa mita 145 hadi 175 na kina cha maji cha mita saba.
Upanuzi wa lango ulifanyika mwaka 1998 ambapo kina kilichimbwa hadi kufikia mita 10.5 na upana wa mita 140 kwa gharama ya Dola za Marekani 240 milioni.
Hata hivyo alisema hivi sasa lango linaruhusu meli zenye ukubwa usiozidi mita 234.
Kutokana na utekelezaji wa mradi wa kupanua na uwekaji wa taa katika lango kuu, pamoja na uchimbaji ndani ya Bandari mwaka 1998, meli zinaweza kuingia usiku na mchana, ukubwa wa meli umeongezeka hadi kufikia urefu wa mita 234/240 na kina cha maji kimeongezeka hadi kufikia mita 10.5.

No comments: