BUNGE LAMALIZA UTATA WA VIWANJA UFUKWE WA LINDI



Mradi mkubwa wa kupima viwanja katika ufukwe  mjini Lindi unadaiwa kugubikwa na utata, hali ambayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeingilia kati na kutaka mchakato huo usitishwe kwa muda.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Hamisi Kigwangala alisema jana bungeni mradi huo unaoendeshwa na Taasisi ya Utility Trust of Tanzania (UTT), wananchi wamenyang’anywa maeneo yao ya asili bila ridhaa yao, kuyapima na kuyauza kwa ujanja ujanja.
Dk Kigwangala alikuwa akiwasilisha taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2014/15 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha ujao.
Kwa mujibu wa Kigwangala, mwananchi mwenye ekari 20 za ufukweni amejikuta akipewa fidia kwa ekari nne na nyingine kuandikishwa majina ya watu wasiojulikana.
“Mheshimiwa spika, kamati imesikitishwa na hili na imeazimia kuitaka Serikali kuwasilisha ndani ya wiki moja taarifa ya namna ilivyolishughulikia jambo hili na hatua ilizochukua dhidi ya udhalimu huu mkubwa kwa wananchi,” alisema.
Aliendelea kusema, “sambamba na hilo, kamati imeiagiza serikali isitishe zoezi hili kwa muda mpaka ukweli wa namna jambo hili lilivyotekelezwa utakapopatikana.”
Hata hivyo, Kigwangala alisema kamati imefurahishwa hatua za awali na za haraka zilizochukuliwa na serikali kutii agizo la kamati.
Kamati hiyo ya bunge kupitia kwa mwenyekiti wake, ilisisitiza, “tusikubali kuvunja misingi imara ya taifa letu kwa kuukubali ubepari na ubeberu kuingia nchini, na hadi kwa wananchi wetu huko vijijini bila kuweka mifumo ya kulinda maslahi yao na kuyasimamia ilhali tunaujua uwezo wao kielimu, kiuchumi na kisheria kuwa ni mdogo.”

No comments: