KKKT WALAANI MLIPUKO WA BOMU MWANZA



Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, limelaani kulipuka kwa bomu katika usharika wa Kanisa Kuu Imani, eneo la Nyumba ya Kupumzikia na Kusababisha mtu mmoja kujeruhiwa.
Kauli ya kulaani kitendo hicho, imetolewa jana naAskofu wa KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrew Gulle, wakati akizungumza na waandishi wa habari kanisani hapo jana.
Askofu hiyo ametoa mwito kwa Serikali kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo ili kuwabaini na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Serikali ihakikishe inatokomeza mtandao huu waugaidi kabla haujaota mizizi na kuondoa amani tuliyoizoea katika nchi yetu,” alisema Gulle.
Alisema baada ya bomu hilo kulipuka usiku wa kuamkiajuzi lilimjeruhi mhudumu wa nyumba hiyo ya kupumzikia wageni, Bernadetha Alfred (25)  katika sehemu mbalimbali za mwili wake miguuni na  usoni ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando na kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo, Askofu huyo ametoa wito kwa Wakristo wote kuwa watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi yanayotendeka.
Alisema tukio la kulipuka kwa bomu katika eneo lakanisa ni la kwanza kwa mkoa wa Mwanza, lakini yalikwishatokea katika kanisa la KKKT Mbagala pamoja na kule Arusha lakini hana uhakika kama lililotokea Mwanza ni mwendelezo wa matukio hayo.
Alisema kwa hivi sasa wanafanya tathmini ya ulinziwa kanisa na kuyaomba makanisa yao yote kuboresha na kuimarisha ulinzi wa maeneo yao.

No comments: