VYAMA VYA TUMBAKU VYATAKIWA KUTUMIA BENKIVyama vya msingi vya wakulima wa zao la tumbaku wilayani Kahama mkoani Shinyanga, vimetakiwa kushirikiana na taasisi za kifedha zikiwemo benki ili waweze kupata mikopo kwa haraka, itakayokuza mitaji yao ya biashara kurejesha kwa wakati uliopangwa.
Meneja  Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa Kitengo ya asasi ndogondogo za kifedha,  Raymond Urassa alitoa  mwito huo wakati akitoa msaada wa mifuko100 ya saruji, yenye thamani ya Sh milioni mbili kwa Chama cha Msingi cha Tumbaku cha Kangeme Kaya ya Ulowa.
Msaada huo una lengo ya kujenga wadi ya wazazi na wajawazito katika kata hiyo.
Urassa alisema benki ya CRDB kwa sasa imeanza kushirikiana  na vyama vya msingi, hasa vile vya wakulima wa tumbaku, lengo likiwa ni kurudisha kiasi
kidogo cha sehemu ya faida wanayopata kwa ajili ya shughuli za kijamii kwa wananchi.
Alisema kuwa ili vyama vya msingi viweze kuendelea, lazima wakulima washirikiane na kuonesha umoja wao, hasa wakati wa kurudisha madeni ya pembejeo wanazokopa katika taasisi mbalimbali za fedha, hususani katika benki.
Pia, Meneja huyo aliwataka wakulima kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kudhibiti wale ambao wamekuwa wakitorosha pembejeo ili kukimbia madeni, waliokopeshwa na vyama vya msingi katika eneo husika.
Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu, John Duttu alisema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka.
Alisema kutokana na msaada huo, wananchi wa eneo hilo hawana budi kujenga kwa nguvu zao hadi kufikia lenta na Halmashauri ya Wilaya itamalizia kwa kuezeka jengo hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ulowa, Paschal Mayengo alisema msaada uliotolewa na benki ya CRDB utakuza uhusiano mzuri na wakazi wa kata hiyo na kukamilika kwa wadi hiyo, kutanufaisha wakazi 25,000 wa eneo hilo.

No comments: