CDA YAENDESHA ZOEZI LA BOMOABOMOA MLIMWA KUSINIMamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imeendesha  zoezi la kubomoa nyumba  eneo la Mlimwa Kusini, karibu na yalipo majengo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Manispaa ya Dodoma. 
Kwa mujibu wa Msemaji wa CDA, Anjela Msimbila wameendesha zoezi hilo juzi baada ya notisi za kuhama za siku 90 kumalizika. Alisema kwamba uvunjaji huo, ulifanyika kwa amani huku wengine wakiwasaidia. 
Alisema watu waliobomolewa nyumba zao, walishapewa viwanja. Takribani nyumba 65 zilibomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara eneo hilo. 
Pamoja na Msemaji wa CDA kusema kwamba kazi hiyo ilifanyika kwa mujibu wa sheria, baadhi ya wakazi walisema kwamba wameshtushwa na sasa hawana makazi. 
Inaaminika kwamba watu 150 wameathiriwa na  shughuli hiyo ya bomoa bomoa.
Wakazi hao walisema wanasikitishwa na kitendo cha kushtukizwa na kubomolewa, huku wengi wao wakiwa hawajatoa vitu vyao ndani na vibaka wakitumia nafasi hiyo, kukwapua vitu vya watu kwa visingizio vya kusalimisha vitu vya watu ambao hawakuwepo nyumbani wakati huo. 
Mmoja wa mabalozi wa nyumba kumi, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema anasikitishwa na tukio hilo, linalowarudisha katika umasikini wananchi waliosota kwa muda mrefu kutafuta kwa kujinyima na kufanikiwa kupata vitu hivyo, japo ni vichache kwa ajili ya familia zao.
Alisema uvunjaji huo, ulikosa utu, kwani wabomoaji hawakuweza kuacha hata nyumba moja walioikuta, ikiwa haina mtu  na kutoa mfano wa nyumba iliyokuwa na watoto 5 wanaoishi peke yao na huku wazazi wao wakiwa safarini, ilivyovunjwa na kuwaacha watoto hao wakihangaika.
 Mwananchi Mwingine, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mgoile, alisema nyumba 65 zilizobomolewa, zina watu zaidi ya 150 kutokana na nyumba moja kuishi familia tatu mpaka tano na wote hawana makazi, kutokana na zoezi hilo la kushtukizwa.
Mtu huyo alihoji kwanini Mwenyekiti wao, asiitishe mkutano na kuwajulisha watu wote ili waondoe vitu vyao.
‘’Hawa watu wana uelewa sana, ona hamna fujo wala malalamiko yoyote katika zoezi zima, hivi kweli kama huyu mama Mwenyekiti angetuita kwenye mkutano na kutuambia, tungeacha kuhamisha vitu na kubomoa wenyewe ili kuondoa mbao na bati?’’ Alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Zubeda Haji alisema yeye hawezi kuzuia maendeleo yanapokuja na kwamba nyumba hizo zote zilizobomolewa, tayari wamiliki wake walishapewa viwanja vingine, wakajenge ili kupisha barabara inayotarajiwa kujengwa baadaye.

No comments: