MTUHUMIWA WA MAUAJI BUTIAMA KUFIKISHWA KORTINI



Jeshi la Polisi mkoani Mara limesema kuwa linakamilisha taratibu za kisheria, ili liweze kumfikisha mahakamani mtuhumiwa wa mauaji, anayedaiwa kuua mwenzake kwa kumpiga na rungu wakiwa kwa mpenzi wao, ambaye wamekuwa wakifanya naye mapenzi kwa pamoja. 
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ferdinand Mtui alisema jana kuwa jeshi hilo linakamilisha taratibu za kisheria ili kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Mtui aliwaondoa wasiwasi wanafamilia ya marehemu Chacha Silasi, aliyeuawa kwa kupigwa na rungu na mtuhumiwa huyo, Boniphace Wankuru Magabe, ambaye alidai walikuwa wakifanya mapenzi wote kwa pamoja na mke wa mtu. 
Alisema kuwa baada ya taratibu hizo kukamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma zinazomkabili. 
“Baada ya taratibu kukamilika tutamfikisha Mahakamani….lakini pia ndugu wa marehemu watupe ushirikiano, hasa wale walioshuhudia mtuhumiwa akimshambulia marehemu,” alisema. 
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumpiga kwa rungu mwenzake Februari 6, mwaka huu usiku katika Kijiji cha Wegero wilayani Butiama, na kusababisha kifo chake Februari 8, akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, alikokimbizwa kwa matibabu. 
Polisi walisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo, alitoroka, lakini alikamatwa Machi 31, mwaka huu. Aliachiwa kwa dhamana Aprili 23, akiwa katika Kituo cha Polisi Butiama.
Ilidaiwa kuwa baada ya kuachiwa, alikwenda kijijini kwake na kutambia ndugu wa marehemu kwamba hawezi kufungwa wakati akiwa na fedha, hali ambayo ilifanya  wanafamilia hao kulalamika na ndipo akakamatwa tena Aprili 28, mwaka huu. 
Aidha, wanafamilia hao walidai kuwa licha ya kukamatwa tena, mtuhumiwa huyo hajafikishwa mahakamani na bado yupo katika Kituo cha Polisi Butiama, jambo ambalo linawatia shaka kwamba kuna mchezo mchafu unataka kuchezwa. 
Hata hivyo, Mtui alisema mtuhumiwa huyo bado anafanyiwa mahojiano zaidi, ikiwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za kisheria ili aweze kufikishwa mahakamani.

No comments: