VITUO VYA MAFUTA KUFUNGWA MASHINE ZA ELEKTRONIKI

Baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha matumizi ya mashine za kielektroniki za utoaji wa risiti (EFDs) kwa wafanyabiashara ndogo na wa kati, sasa imevigeukia vituo vya mafuta kwa kuwaanzishia utaratibu wa kufunga mashine za kielektroniki za utoaji wa risiti kwenye pampu zake.
Tayari muda wa mwisho kutekeleza agizo hilo umefikia Aprili 30 mwaka huu na kuanzia Mei Mosi vituo vyote nchini vimetakiwa kufunga mashine hizo ambapo kila pampu itakapomaliza kutoa mafuta hapohapo  itatoka risiti kwa mteja inayoonesha kiwango cha mafuta kilichouzwa na gharama zake.
Akizungumza kwenye mafunzo kwa wanachama wa Mtandao wa waandishi wa habari za kodi Tanzania (TAWNET) jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema walivipa barua vituo vyote vya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini kuhusu suala hilo.
“Kabla ya muda wa mwisho tulianza majaribio kwa baadhi ya vituo na tunaona mafanikio mfano kituo cha Engen cha Mbezi Beach.
“Baada ya muda huo tutaanza ukaguzi, lakini wenye mafuta wametueleza gharama kubwa kufunga mashine moja kwa kila pampu hivyo wakati utaratibu unaanza wa kutumia mashine nasi tunaendelea kufanya nao mazungumzo tuone kama inawezekana mashine moja kufungwa kwenye pampu zaidi ya moja mfano kituo cha mafuta cha Victoria kina pampu 20 inakuwa vigumu kuweka mashine kote,” alisema.
Mfumo wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na awamu ya pili ulianza mwaka 2013 ikiwahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT na wenye mauzo ghafi  kwa mwaka ya Sh milioni 14 na zaidi. Lengo ni kusajili wafanyabiashara 200,000.
Naye Meneja Madeni na Makusanyo wa TRA, Matilda Kunenge alisema katika kuwazuia wananchi kuwa na Namba ya Mlipakodi (TIN) zaidi ya moja na kutumika katika kukwepa kodi, kila mwenye TIN na waombaji wapya wanachukuliwa alama zao za vidole.

No comments: