NEEMA YAZISHUKIA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA

Serikali imesema imejipanga kuongeza uwekezaji katika Shule za Sekondari za Kata nchini ili kuongeza kiwango cha ufaulu ambapo pia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa  katika sekta ya elimu umesaidia kuinua kiwango cha ufaulu kidato cha nne ambacho kilitetereka kwa miaka mitatu mfululizo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda  wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Elimu Tanzania uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa.
Alisema takwimu zinaonesha  wastani wa ufaulu wa shule za kata ni mdogo, ambao ni sawa na asilimia 48, ikilinganishwa na asilimia 59.7 ya shule za serikali kwa kipindi cha mwaka jana. Pia alisema idadi ya wanafunzi waliofaulu kidato cha nne kwa mwaka  jana wengi wao walitoka shule za kata kutokana na shule hizo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
“Serikali itajipanga kuhakikisha inaongeza uwekezaji kwenye shule za kata  na zile za vipaji maalumu hasa katika kuboresha miundombinu ili kuongeza kiwango cha ufaulu,” alisema.
Waziri Mkuu alisema taarifa za matokeo ya kidato cha nne  zinaonesha ufaulu  wa juu kuanzia daraja la kwanza hadi tatu kwa mwaka 2013 unaonekana kuwa mkubwa ukilinganisha na miaka ya 2010, 2011 na 2012 kwa shule za kata, serikali, binafsi  na seminari.
Alisema idadi ya wanafunzi wengi waliofaulu katika mitihani hiyo ni kutoka shule za kata ambao ni 109,229 ikilinganishwa na 52,242 wa shule binafsi, 33,533 wa shule za serikali na 6,149 wa shule za seminari.
Aidha, takwimu zinaonesha ufaulu usioridhisha wa daraja la 0 kwa shule za kata kwa mwaka 2013 ni wa chini kuliko miaka mitatu iliyopita.
Alisema ufaulu wa daraja hilo mwaka 2013 ulikuwa asilimia 51.80, mwaka 2012 ilikuwa asilimia 56.9, mwaka 2011 ilikuwa asilimia 57.4 na mwaka 2010 asilimia 64.6 na kupungua kwa ufaulu huo kumechangiwa na kuongezeka kwa ufaulu wa shule hizo kwenye daraja la  kwanza, pili, tatu na nne.
Waziri Mkuu alisema kuanzishwa kwa Mpango wa Matokeo Makubwa kumeleta ushindani kwa kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu na kutoa tuzo kwa shule 3,000 zilizofanya vizuri na zinazoonesha kupiga hatua katika mitihani ya mwaka 2013.
Alisema mpango huo umeimarisha usimamizi na menejimenti ya shule kwa kuandaa kitabu cha kiongozi na kutoa mafunzo kwa wakuu wa shule za sekondari 3,000 aidha umejenga uwezo wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kutoa mitihani ya majaribio kwa darasa la sita na saba katika elimu ya msingi na kidato cha nne kwenye elimu ya sekondari na kusimamia uimarishaji wa miundombinu ya shule 264.
Alisema hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, miundombinu kwa shule 56 kati ya shule 264 ilikuwa imekamilika.
Pia Waziri Mkuu pia alizitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinatumia vizuri fedha zilizotengwa katika masuala ya elimu na Mkurugenzi yeyote atakayetumia vibaya fedha hizo atawajibishwa.
Waziri Mkuu alisema serikali imepanga kupunguza tatizo la walimu hususani wa masomo ya sayansi na hisabati kwa kutumia  mwalimu mmoja mahiri katika shule ya kufundishia  madarasa mengi  kwa wakati mmoja.
Alisema mpango huo umeandaliwa ili utumie  gharama nafuu na utaanza kutumika Juni mwaka huu.
Aidha, Waziri Mkuu alisema shule za msingi nchini zinakabiliwa na upungufu wa madawati karibu milioni moja na nusu, ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ijifunge mkanda na kulipa kipaumbele suala la kupunguza tatizo hilo.
“Takwimu nilizonazo zinaonesha kuwa Tanzania ina mahitaji ya madawati 3,302,678 wakati madawati yaliyopo ni 1,837,783 kwa hiyo tuna upungufu wa madawati 1,464,895 katika shule zetu za msingi,”  alisema Waziri Mkuu.
Kutokana na mahitaji hayo, Waziri Mkuu alisema endapo Serikali itaamua kutengeneza madawati 100,000 kwa mwaka kwa gharama ya Sh bilioni 12, itachukua miaka 15 kumaliza tatizo hilo ili kuziba pengo lililopo sasa.
“Nimepita kwenye banda la Taasisi ya *Maajar Trust* na pale wameniambia kuwa wameshatengeneza madawati 12,000 na kuyagawa katika mikoa sita. Wastani wa kila dawati ni Sh 120,000 lakini inategemea na upatikanaji wa mbao pamoja na gharama za ufundi.”
“Tukichukua gharama zao, tukaamua kutengeneza madawati 200,000 kwa mwaka, itatugharimu Sh bilioni 24 na itachukua miaka saba kumaliza tatizo hilo wakati tukiamua kutengeneza madawati 300,000 kwa mwaka, itatugharimu Sh bilioni 36 na itachukua miaka mitano kumaliza tatizo hilo,” alifafanua Waziri Mkuu.
Alisema ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kumaliza tatizo hilo kwani inatia aibu na hakuna sababu ya kuendelea kuona wanafunzi wakisoma huku wamekaa chini.
“Waziri wa Elimu na watu wako ni lazima mjifunge mkanda na kipaumbele chenu kiwe ni kupunguza tatizo la madawati katika muda mfupi sana; na itakuwa vema kama mtajipanga haraka ili mje na suluhisho ndani ya wiki hii kabla Mheshimiwa Rais hajaja kufunga maonyesho haya,” aliongeza.
"Kaeni na watu wa Taasisi ya *Maajar Trust* muone ni kwa njia gani mnaweza kutatua tatizo hili… kama ni kuandaa chakula cha hisani ili kuchangia madawati fanyeni hivyo ili tatizo hili liishe. Wako Watanzania wanaweza kuchangia dawati moja, mawili, matatu au zaidi na tukajikuta tumemaliza tatizo hili,” alisema.

No comments: