AUA MKEWE MJAMZITO AKIDAI NI MVIVU WA KULIMA

Mjamzito Agatha Isack (19) amekufa kwa kipigo kutoka kwa mumewe akisaidiwa na mwanamke anayeaminika kuwa hawara yake, akimtuhumu  kuwa mvivu  wa kulima shambani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa mama huyo mjamzito ambaye ni mkazi  wa kijiji  cha Manga, Kata ya Kasokola  wilayani Mlele  alifikwa na umauti  akikimbizwa katika zahanati  kijijini  hapo kwa  matibabu.
Inadaiwa  baada ya hali  yake  kubadilika  ghafla  kutokana na kipigo kutoka kwa mumewe  Vitus Mlengo (23), mume alikodisha pikipiki  na kumkimbiza  kwenye  zahanati, lakini  alikata  roho akiwa njiani.
Akielezea mkasa  huo  unaodaiwa  kutokea juzi saa sita mchana nyumbani  kwa wanandoa  hao  kijijini humo,  Kamanda Kidavashari alisema awali baada ya kipigo mwanamke huyo alikwenda katika  zahanati  iliyopo kijijini  humo kwa uchunguzi  zaidi  na matibabu.
Kabla ya kufika hospitalini alikwenda kwa  mama yake mdogo  aitwae Anastazia Charles  na kumsimulia jinsi  alivyopigwa  na mumewe akishirikiana  na Faustina Matheo (31) ambaye anadaiwa  kuwa na mahusiano  ya kimapenzi  na Mlengo.
“Baada ya kutibiwa Agatha  alipitia  nyumbani  kwa bibi yake kijijini humo  na kumweleza  jinsi alivyopigwa na mumewe  pia alimfahamisha bibi  yake  kuwa mumewe  alimuonya  asirudi  nyumbani  bila mboga  hivyo  bibi  yake  huyo  alimpatia  mboga  naye  akarejea  kwake,“ alibainisha Kamanda Kidavashari.
Inadaiwa alipofika nyumbani  kwa  mumewe, Mlengo alimfukuza ndipo  alirudi  kwa bibi  yake  na kulazimika  kulala  nyumbani  kwake  hadi asubuhi  ya siku iliyofuata ambapo  Agatha  alifuatana  na  bibi  yake  huyo  ndipo  mumewe  akakubali  kumpokea .
Kidavashari alifafanua kuwa juzi, saa mbili  usiku Agatha  alishindwa kula  chakula  alichokipika  mwenyewe  akilalamikia kuhisi  maumivu makali  kichwani  ndipo  mumewe alipoona  hali yake  imebadilika  ndipo  alilazimika  kuomba msaada   wa pikipiki  kwa rafiki yake aitwae Alfred Kasonso  na kumkimbiza  katika zahanati  kijijini  humo kwa matibabu .
Kamanda alithibitisha kuwa mume wa marehemu huyo na Faustina  wanashikiliwa na Polisi  kwa mahojiano.
Katika tukio lingine,  mwendesha  pikipiki ‘bodaboda', Daniel Kapufi (20)  mkazi  wa  mjini Sumbawanga  mkoani Rukwa  ameuawa  kikatili kwa  kukatwa katwa  na shoka na mapanga  baada ya ‘kunaswa’  akisafirisha  nyama ya  ng’ombe  inayodaiwa kuwa  ya wizi akitumia  pikipiki  yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana  saa tisa usiku katika kitongoji cha Malangali, Manispaa ya Sumbawanga.
Mtendaji wa Kata ya Malangali, Basil Stima, alisema kuwa chanzo cha kijana huyo kuuawa ni kutokana na kunaswa akisafirisha nyama ya ng'ombe kwa kutumia usafiri wa pikipiki yake, ng’ombe  anayedaiwa   kuibwa na kuchinjwa   katika msitu  karibu na  kitongoji hicho  cha Malangali.
Alisema kuwa baada ya bodaboda huyo  kubeba furushi la kwanza  la nyama hiyo, alirudia mzigo wa pili ndipo aliponaswa na kundi la watu ambao  walimhoji  alikoitoa nyama hiyo ambapo wakati  akijieleza   ghafla  walianza kumshushia kupigo huku  wakitumia silaha mbalimbali ya jadi,  yakiwemo  mapanga na  kumsababishia  umauti  kisha wakaichoma moto pikipiki  yake.

No comments: