BOMANI ASHANGAA WANAOTAKA KUKIMBILIA MSITUNI KATIBA MPYA

Jaji mstaafu Mark Bomani amewashangaa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaodai kuwa wasipopata Katiba mpya watakwenda msituni na kuhoji wanakwenda huko kufanya nini wakati msituni ni kwa ajili ya wanyama na si binadamu.
Bomani alionesha mshangao huo wakati akihutubia wanahabari waliokutana jana jijini hapa kuadhimisha Siku ya  Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Alisema wapo wabunge wanahitaji kuelimishwa na kama wana mawazo yao wawatumie wanahabari ili waweze kuyatoa, lakini si kudai kuwa wasipopata Katiba mpya wataenda msituni.
“Msituni wanamfuata nani, msituni ni kwa ajili ya wanyama, watu hawakai msituni, huyo anayekwenda msituni familia yake ataitelekeza wapi,” alihoji Jaji Bomani na kuongeza kuwa mtu anayefikiria hivyo anahitaji kusaidiwa kama ana mawazo anayotoa yaandikwe lakini kwenda msituni hakuwezi kusaidia kitu.
Kwa mujibu wa Jaji Bomani, tasnia ya habari ina wajibu wa kuielimisha jamii na sio masuala ya Katiba pekee ila mambo ya kimaendeleo, kwani nia ni kumwendeleza Mtanzania katika maisha yake ya kila siku.
Akizungumzia mwenendo wa mchakato wa Katiba, alisema lengo  ni  kupata katiba ambayo ni bora zaidi kuliko ile iliyopo sasa itakayosaidia kushughulikia changamoto, itakayotengeneza mazingira ya haraka zaidi ili kuleta maendeleo, huku akiwataka wanahabari kuwajibika kwa kuelimisha umma juu ya mambo muhimu yalipo ndani ya Katiba hiyo na kama yana faida gani.
Akizungumzia juu ya muswada wa  tansia ya habari, alisema inatia aibu kwa miaka zaidi ya 10 muswada huo umekwama na kuhoji ni  kwa nini umekwama na kuongeza kuwa kutopitishwa kwa muswada huo kusiwakatishe tamaa ila wapambane ili kuhakikisha Sheria hiyo inafika bungeni.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari nchini (TAMWA), Valerie Msoka aliwasihi wanahabari wachanga kutokata tamaa na kuamua kuchepuka bali waone changamoto wanazozipata kuwa ni sehemu ya maisha itakayoweza kupata kujulikana zaidi kutokana na habari wanazoziandika.

No comments: