UPELELEZI WA MAUAJI KWENYE GHOROFA LILILOPOROMOKA BADO



Upelelezi wa kesi ya mauaji ya watu 27 yaliyotokea baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime na wenzake 11, haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Bernald Kongolo alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Devotha Kisoka aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 9 mwaka huu itakapotajwa tena kuangalia kama upelelezi umekamilika. Wakati huo washitakiwa wote wanaendelea kubaki rumande kwa kuwa mashitaka yao hayana dhamana.
Mbali na Fuime washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mfanyabiashara Laza Radha, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed (59), watendaji katika Manispaa ya Ilala akiwemo Mhandisi Mkuu, Charles Ogare (48), Mhandisi Majengo, Godluck Sylivester (35) na Mkurugenzi Mkuu wa Ukaguzi wa Majengo, Willibrod Mugyabuso (42).
Wengine ni Mhandisi, Mohamed Abdulkarim (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoshaodaga Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo (60), Mkadiriaji Ujenzi, Vedasto Ruhale (59) na Msanifu Majengo, Michael Hema. 
Inadaiwa kuwa Machi 29 mwaka jana, katika mtaa wa India Gandhi Ilala, Dar es Salaam kwa makusudi washitakiwa waliwaua watu 27.
Hivi karibuni Fuime aliiomba Mahakama imfutie mashitaka ya mauaji, lakini Hakimu Kisoka alisema hawezi kutoa uamuzi kwa kuwa jalada la kesi lipo Mahakama Kuu.
Awali, washitakiwa hao isipokuwa Fuime walikabiliwa na mashitaka ya kuua watu 24 bila kukusudia. Baadaye walibadilishiwa mashitaka na kuwa ya kuua kwa kukusudia na kuunganishwa na mkurugenzi huyo.

No comments: