WAZIRI MKUU ATETEA MBIO ZA MWENGEWaziri Mkuu, Mizengo Pinda ametetea umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, akisema ni jambo kubwa lenye manufaa ambalo moja ya faida zake ni kuhimiza umuhimu wa kujitolea miongoni mwa wananchi katika kujiletea maendeleo yao.
Aidha, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amesema mbio za Mwenge zinaeneza ujumbe wenye manufaa kwa jamii, kuliko mikutano inayofanywa na kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Waziri Mkuu Pinda alishangazwa na mjadala ulioibuliwa na wabunge wa upinzani bungeni jana kuona Mwenge kama suala lisilo na maana kwa taifa.
“Nimesimama kwa sababu nimesikiliza mjadala hapa, naona jambo hili kubwa, linaonekana kama halina maana kwa taifa,” alisema Pinda na kuongeza:“Kila mwaka, mbio za Mwenge huwa na kaulimbiu mahsusi kwa sababu Mwenge huu huwa na fursa ya kufika maeneo mengi hivyo kufikisha ujumbe kuhusu masuala mazito ya nchi kama elimu. Kwa hiyo, si sahihi kabisa kuona Mwenge hauna maana.”
Alisema anafahamu kuwa wapinzani wanaweza wasipendezwe sana na Mwenge kuhimiza suala la kujitolea miongoni mwa wananchi.
“Hili linaweza lisiwapendeze sana wenzetu wa upande wa pili. Mwenge unahimiza suala la kujitolea katika shughuli zao za maendeleo. 
“Wananchi wanahimizwa kuenzi moyo huo na wamekuwa wakifanya hivyo katika shughuli mbalimbali za kijamii. Hili halina ukakasi hata kidogo. 
“Hoja hapa imekuwa ni michango, lakini hivi Mwenge unakuja pale kwangu Kibaoni, kwa ugeni huo, unaofanya kazi nzuri, kama watu wanachanga kuku, bata, hii siyo dhambi. Wananchi wamekuwa wakarimu sana katika jambo hili,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema), alitaka kufahamu ni kiasi gani cha fedha hutumika kwa kila wilaya kwa ajili ya mbio za Mwenge, gharama za kuuwasha na kuuzima na faida zinazopatikana.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Nkamia alisema Serikali hutenga fedha kulingana na mahitaji ya gharama halisi ya wakati husika.
Alitoa mfano wa mwaka 2012, Sh milioni 650 zilitengwa kwa ajili ya kuadhimisha uzinduzi na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru; ambazo kati ya hizo, Sh milioni 450 zilitumika na Wizara na Sh milioni 200 zilitumika na mkoa mwenyeji wa kilele cha mbio hizo.
Kuhusu faida, alitaja kuwa ni kuendelea kutunza historia na falsafa ya ukombozi wa taifa, kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuenzi amani, mshikamano, upendo na zaidi kupambana na aina yoyote ile ya kuwabagua Watanzania kwa rangi, dini au makabila yao.
Pia kuendelea kuhamasisha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kujiletea maendeleo.
Hata hivyo katika maswali ya nyongeza, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema Mwenge unaongeza ugumu wa maisha kwa kuchangisha wananchi na kuwa viongozi wa mbio hizo mwaka huu wanapita kupiga propaganda ya serikali mbili na kutaka mbio hizo zifutwe.
Akijibu swali hilo, Nkamia alisisitiza kuwa Serikali haiko tayari kusitisha mbio hizo, kwani wananchi wana imani nazo na zimesaidia kudumisha umoja na amani. Alisema Mwenge unatoa ujumbe mzuri kuliko  unaotolewa na Ukawa.
Mbali ya Mnyika, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alihoji sababu za walimu kulazimishwa kuchangia mbio hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema michango hiyo ni hiari na hakuna anayelazimishwa kuchangia, na kwamba hailipii mafuta ya Mwenge wala posho za wakimbizaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), yeye aliitaka Wizara iongeze siku za kukimbizwa Mwenge wilayani Kishapu kwani una manufaa makubwa, na Wizara imeahidi kulifanyia kazi ombi hilo huku ikipongeza hatua hiyo.
Baada ya hapo, Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi zaidi, lakini baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu, wabunge wa upinzani walisimama tena na kuomba Mwongozo kuhusu majibu hayo ya mawaziri.
Waliosimama ni Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), Moses Machali (NCCR-Mageuzi – Kasulu Mjini) na Susan Kiwanga (Viti Maalumu – Chadema), wote wakieleza kuwa wananchi wanachangishwa, na baadhi yao kusoma ujumbe waliotumiwa katika simu zao za mkononi.
Naibu Spika Ndugai alisema atatoa majibu ya miongozo hiyo ‘mbele ya safari.’

No comments: