MTAALA KUBADILISHWA KUPUNGUZA MIMBA ZA UTOTONISerikali inatarajia kuweka katika mtaala wa elimu unaotumika sasa, somo la afya ya uzazi kwa vijana katika shule za msingi na sekondari nchini kupunguza mimba za utotoni na maambukizi ya Ukimwi.
Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama katika ufunguzi wa mkutano wa siku tatu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana uliozishirikisha nchi 16.
Mhagama alisema serikali imeweka mikakati ya kuanzisha elimu hiyo ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana katika shule za msingi kutokana na ukubwa wa tatizo la mimba za utotoni na maambukizi ya Ukimwi.
“Serikali inawahakikishia wanasayansi kuwa elimu hiyo itawapa matokeo chanya kwamba hakutakuwa na maambukizi wala mimba za utotoni kwa vijana hao,’’ alisema Mhagama katika hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa masuala mtambuka katika wizara hiyo, Letisia Sayi.
Mhagama alisema elimu ya afya ya uzazi kwa vijana itasaidia kubadili tabia, kujikinga kwa kutumia kondomu na wanaoishi na maambukizi kulinda afya zao.
Naye, Mtaalamu wa kitaifa wa masuala ya Ukimwi na elimu ya afya wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Martin Herman alisema takwimu za wizara hiyo zinaonesha wanafunzi 6000 kila mwaka wanaacha shule kwa sababu ya mimba za utotoni.
Herman alisema mpango huo wa kutoa elimu ya afya utaanza Julai mwaka huu  baada ya mapitio ya mtaala huo na inatarajiwa ifikapo mwaka 2015 wanafunzi watajua afya ya uzazi na kupata walimu waliobobea katika masomo hayo.
Nchi zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Sweden, Uganda, Malawi, Zimbabwe, Zambia, Burundi, Namibia, Rwanda, Botswana, Lesotho, Swaziland, Angola, Ethiopia na wenyeji Tanzania.

No comments: