UJENZI WA KIVUKO DAR-BAGAMOYO KUKAMILIKA MWEZI UJAO


Serikali imetangaza kununua kivuko kipya kitakachofanya kazi kati ya Magogoni – Kigamboni, jijini Dar es Salaam na Pangani na Bweni mkoani Tanga, huku ujenzi wa kivuko kitakachotoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, ukitarajiwa kukamilika mwezi ujao nchini Bangladesh. 
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema hayo juzi usiku wakati alipowasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo bungeni, ambako aliomba aidhinishiwe Sh trilioni 1.22. 
Kuhusu kivuko cha kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, Dk Magufuli alisema; “ujenzi wa kivuko kitakachotoa huduma za usafiri kati ya Dar es Salaam na mwambao wa Bahari ya Hindi hadi Bagamoyo unaendelea nchini Bangladesh ambapo kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni, 2014.” 
Akizungumzia ununuzi mpya wa vivuko, alisema katika mwaka wa fedha 2014/15 zimetengwa Sh bilioni 4.5 kwa ajili ya kazi hizo, ikiwamo kununua kivuko kati ya Magogoni – Kigamboni (Sh bilioni 3.9), ununuzi wa mashine za kukatia tiketi kwa ajili ya vivuko vya Kisorya, Ilagala na Pangani (Sh milioni 150). 
Alisema pia kutafanyika ununuzi wa vifaa vya karakana za Temesa katika mikoa ya Manyara, Singida, Lindi, Mwanza, Kagera na Ruvuma, pamoja na kufuatilia miradi hiyo. 
Dk Magufuli alisema kutafanyika ukarabati wa vivuko vya Mv Magogoni, Mv Mwanza, ‘Tug boat’ Mv Kiu – Morogoro, na Mv Pangani II. Alisema ujenzi wa kivuko cha Mv Malagarasi mkoani Kigoma, ulikamilika na kuzinduliwa Oktoba 25, 2013 na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal. 
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli alisema wizara inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa barabara mbadala kati ya Dar es Salaam na Chalinze kwa kiwango cha Expressway na itakuwa ya kulipia yenye njia sita. 
Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 100, itajengwa kwa utaratibu wa kushirikisha Serikali na Sekta Binafsi (PPP). 
“Barabara hiyo mbadala ambayo itakuwa ni ya kulipia, itajengwa kwa njia sita (6 lanes). Barabara iliyopo sasa itaendelea kutoa huduma kwa wale ambao hawako tayari kutumia barabara ya kulipia,” alisema Dk Magufuli na kuongeza: 
“Wizara imefanya maandalizi ya ujenzi wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa awali (pre-feasibility study), kutoa tangazo la kualika kampuni kuonesha nia (Expression of Interest) ya kushiriki katika ujenzi wa barabara hii kwa utaratibu wa PPP ambapo kampuni 12 zimeonesha kuwa na uwezo wa kujenga barabara hiyo.” 
Alisema Wizara inaendelea na taratibu za kumpata Mtaalamu Mwelekezi wa mradi ambaye ataisaidia Serikali katika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu, kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata mbia pamoja na kushauri masuala ya kifedha na kisheria.

No comments: