TAZARA BADO HAKIELEWEKI LICHA YA KUPATIWA MABILIONILicha ya Serikali kutoa Sh bilioni 1.6 ili kulipa wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), bado wamesisitiza kuendelea na mgomo kwa madai kuwa fedha iliyotolewa ni ya miezi miwili na bado wana madai ya mwezi mmoja.
Akizungumza jana na mwandishi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu), Kanda ya Dar es Salaam, Yusuph Mandai alisema wafanyakazi wamekataa kurudi kazini hadi hapo watakapolipwa fedha yote.
Alisema fedha inayodaiwa kupatikana ni ya miezi miwili pekee, Februari na Aprili na umebakia mwezi mmoja ambao fedha yake haijaingizwa katika akaunti hivyo hawawezi kurudi kazini.
“Fedha inayodaiwa kutolewa wafanyakazi hawajaiweka mifukoni, lakini pia bado mwezi mmoja ambao fedha yake hazikuwekwa,” alisema Mandai.
Alisema wafanyakazi wana nia njema na shirika ila matakwa yao hayajatimizwa kama inavyostahili na kwa wakati.
Aliitaja fedha za miezi iliyotolewa kuwa ni ya Februari na Aprili huku ukibaki mmoja na Serikali ya Zambia inatakiwa kulipa mshahara wa  Machi na Mei.
Mgomo huo ulianza wiki iliyopita kwa madai ya wafanyakazi hao kulipwa mishahara yao.

No comments: