MBUNGE ATAKA TOZO KWA MAGARI YANAYOINGIA KATIKATI YA JIJI


Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu (CCM), ametaka magari yanayoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam,  kutozwa fedha ili kudhibiti msongamano wa magari katika jiji hilo na kuepuka  watu wenye magari wanaoingia bila kuwa na kazi maalumu. 
Zungu alisema hayo bungeni jana, wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi huku akidai kuna magari 50,000 yanaingia katikati ya Jiji kutoka Tegeta kila siku.
“Msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, umekuwa ukikua siku hadi siku, hivyo ni vyema kuwe na tozo ya kuingia katikati ya mji kwa kuwa kuna watu wanakuja mjini kuzurura ikiwemo ‘kupiga mizinga’ (kuomba fedha). Wangekuwa wanalipa wasingeingia mjini na misongamano ingepungua,” alisema. 
Pia alishauri Wizara kuwa na mpango maalum wa kukopesha mkoa huo Sh bilioni 400 za kukarabati miundombinu  iliyoharibika kwa kiasi kikubwa. 
Alisema kwa kuwa jiji hilo linachangia asilimia 80 ya mapato ya Serikali, ni vema kuwe na mpango maalumu  au mkopo utakaowezesha kupata fedha hizo na kukarabati barabara zote na baadae zilipwe na  wananchi wa mkoa huo. 
Kwa mujibu wa Zungu, mkopo huo ungeweza kulipwa kwa kodi za majengo wanazotozwa wananchi, kwani Jiji linakusanya zaidi ya Sh bilioni 25 kwa mwaka hivyo lina uwezo wa kulipa kwa miaka isiyozidi 15. 
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisema kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam linachangia mapato makubwa ya asilimia 80 katika mapato ya Serikali, kunahitajika mkakati wa dharura kukabiliana na uharibifu uliotokana na mafuriko yaliyokabili mkoa huo hivi karibuni.

No comments: