TIGO YAZINDUA TAMTHILIA MPYA KUHUSU BIMA


Kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Tigo  imezindua tamthilia mpya ya ‘Kinga ya moyo wangu’, kwa lengo la kuielimisha jamii juu ya masuala ya bima. 
Tamthilia hiyo ambayo imezinduliwa kupitia Tigo Bima ya mtandao huo,  inalenga kuwaelimisha Watanzania juu ya umuhimu wa kuwa na bima, hasa kutokana na uwiano mdogo uliopo kwa watu wenye bima. 
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez alisema kiwango cha Watanzania waliojiandikisha katika bima kwa hiari, hakiridhishi, kwani ni asilimia moja ya watu wazima ndiyo wamejiandikisha. 
“Kampuni kama Tigo ina wajibu katika kuwapatia wateja wake huduma zenye gharama nafuu, hivi sasa tuko tayari katika hilo kupitia Tigo Bima kwa njia ya simu,” alisema Gutierrez. 
Meneja Mkazi wa kampuni ya Bima Tanzania, Christian Karlander  alisema bima zinaweza kuwa kimbilio salama kwa jamii na familia zao, pale wanapopatwa na matatizo mbalimbali. 
“Kinga ya Moyo wangu ni mradi wa kwanza wa aina yake, unaoelimisha kwa kutumia chombo kama redio kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi, ambao hawajahi kuelimishwa kuhusu bima,” alisema. 
Kipindi hicho kitakuwa kikirushwa mara mbili kwa siku katika redio ya Clouds kwenye vipindi vya Leo Tena na Jahazi.

No comments: