BUNGE LASHAURI MSAMAHA WA KODI KWENYE SUKARI UFUTWE


Serikali imeshauriwa kufuta misamaha ya kodi katika sukari inayoagizwa kuziba pengo, na pia isiendelee kupandisha ushuru katika bidhaa za sigara, bia, mvinyo, vinywaji vikali na baridi. 
Hayo yamo katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara ilipowasilisha bungeni maoni yake kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara.Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Luhaga Mpina, alisema misamaha ya kodi katika sukari haimsaidii mwananchi, bali kikundi cha watu. “Pia gap sugar (sukari ya matumizi ya nyumbani) na industrial sugar (sukari ya viwandani), ziagizwe kwa utaratibu wa bulk procurement (mfumo wa uagizaji wa pamoja) ili kuzuia uagizaji holela na ukwepaji kodi,” alisema Mpina, Mbunge wa Kisesa (CCM).Kamati hiyo ilisema uuagizaji huo wa sukari kwa pamoja ufanywe na kampuni itakayoundwa na wazalishaji sukari watakaolipa kodi stahiki kwa sukari itakayoagizwa ili kulinda viwanda vya sukari na wakulima wadogo wa miwa nchini. 
Kuhusu ushuru, alisema Serikali isiendelee kupandisha ushuru katika bidhaa za sigara, bia, mvinyo, vinywaji vikali na vinywaji baridi na hata kama italazimika, basi ongezeko hilo lisizidi mfumuko wa bei ambao kwa sasa ni asilimia 6.5. 
Aidha, Kamati iliipongeza Serikali kwa kutoa fedha Sh bilioni 8.5 kwa ajili ya kukarabati barabara ambayo inatumika kusafirishia vifaa na mitambo mizito kwenda katika miradi ya Liganga na Mchuchuma. 
Hata hivyo, Kamati ilihoji kwa nini Serikali imeamua kupandisha ada na tozo kwa kiwango cha juu kwa bidhaa za mbao na upimaji wa viwanja. 
Katika maoni yao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliishauri Serikali irejeshe viwanda vyote ambavyo vimefungwa baada ya wawekezaji kushindwa kutekeleza mikataba ya uwekezaji. 
Kuhusu bidhaa feki, iliishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kukamilisha Sheria maalumu ya kudhibiti bidhaa feki na pia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lijengewe uwezo mkubwa kwani lina watumishi wachache, huku likisimamia eneo kubwa la nchi.

No comments: