EWURA YASIFU UBORA WA PETROLI NA DIZELI YA TANZANIA


Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na bidhaa bora zaidi ya mafuta ya petroli na dizeli yenye kiwango kidogo cha kemikali cha salfa na ifikapo Januari mwakani, ubora utaongezeka mara dufu.
Kiwango cha salfa kinachopimwa katika mafuta ya petroli nchini ni 15ppm wakati kwa dizeli ni 500 ppm na imeelezwa na huenda Januari mwakani kiwango cha kemikali hiyo katika dizeli kikashuka hadi 50 ppm.
Kutokana na ubora huo, mafuta ya Tanzania ni salama kwa injini za magari na mitambo mingine, yanapunguza gharama kwa kutotumika sana kwa umbali unaolinganishwa na yenye kiwango kikubwa cha salfa na kupunguza athari za mazingira pamoja na afya kwa jamii. 
Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam katika mkutano wa majadiliano kuhusu faida za kutumia mafuta ya petroli na dizeli yenye kiwango kidogo cha salfa, ikiwa ni hatua ya kupunguza athari za kiuchumi na kijamii kwa binadamu ikiwemo magonjwa ya saratani, kutoka kwa mimba na watoto kuzaliwa kabla ya siku. 
Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Gerald Maganga akitoa mada katika mkutano huo uliowashirikisha wadau wa mafuta nchini, alisema mafuta yenye viwango vikubwa vya salfa yana madhara makubwa na Tanzania kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeweka viwango kupunguza tatizo hilo. 
Alisema kwa hapa nchini TBS imeweka viwango hivyo na kuwezesha mwaka 2012 kutoka 5000 ppm kwa mafuta ya dizeli hadi 500 ppm na ikiwa shirika hilo litapitisha viwango vipya mwakani, kitaanza kutumika kiwango cha 50ppm kwa dizeli. 
Maganga alisema katika mkutano huo ulioandaliwa na Ewura kuwa, lengo ni kuondoa kabisa kemikali za salfa katika dizeli na petroli na hivyo kunusuru afya za wananchi. 
“Matumizi ya mafuta yenye salfa kwa nchi zinazoendelea bado ni makubwa sana, Chile, Costa Rica, Puerto Rico na Kisiwa cha Virgin ni nchi pekee Amerika Kusini na ukanda wa Caribbean zilizopunguza salfa katika dizeli kwa 50ppm. Tanzania kwa Afrika Mashariki tunaongoza kwa matumizi kidogo ya salfa na hivi karibuni tutapunguza zaidi,” alisema Maganga. 
Hata hivyo, Maganga alisema wakati hatua mbalimbali zikichukuliwa, ikiwemo mabadiliko ya viwango, sera na utekelezaji wa sheria, elimu zaidi inahitajika kusaidia watumiaji na wananchi kuelewa athari za salfa katika mafuta na faida za kuondoa kemikali hiyo ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini. 
Kwa upande wake, mdau wa mafuta kutoka kampuni ya ATN Petrolium ya Morogoro, Paulo Lunyalila alisema moja ya faida kubwa ya hali hiyo ni kupunguza magonjwa, watoto kuzaliwa kabla ya muda, kutoharibika kwa injini za magari na mitambo na kupunguza matumizi ya mafuta mengi kwa mwendo wa umbali mdogo.

No comments: