KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI YAAHIRISHWA


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeendelea kuchelewesha kesi ya kuvua samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania bila kibali, inayowakabili raia wawili wa China. 
Hatua hiyo inatokana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Prosper Mwangamila kuomba kesi hiyo iliyotajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iahirishwe kwa kuwa bado wanasubiri nyaraka halisi zilizowasilishwa Mahakama Kuu wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa awali. 
Mwangamila alidai, mara ya mwisho kesi ilipotajwa aliitaarifu mahakama kuwa wanasubiri nyaraka hizo na hadi sasa hawajazipata.
Lakini, alisema  Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu ambaye hakumtaja jina lake, aliwaeleza kuwa kama mambo yatakwenda vizuri mwishoni mwa wiki hii, anaweza akawapa nyaraka hizo.
Wakili wa upande wa utetezi, Kapteni Ibrahim Bendera aliomba kesi hiyo itajwe wiki ijayo ili wajue nini kinaendelea. Alihoji upande wa Jamhuri wanatafuta nyaraka  tu au lah, kwa sababu kuna ushahidi mwingine ulishazama.
Hakimu Waliarwande Lema anayesikiliza kesi hiyo, alisema upande wa Jamhuri umeshatoa mwelekeo wa wazi, kuhusiana na upatikanaji wa nyaraka hizo, hivyo haoni sababu za kuendelea kujadili suala hilo. Aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 28 mwaka huu, itakapotajwa tena.

No comments: